Mlawa aanza safari ya ubunge Kilolo

IRINGA: Mdau wa maendeleo Aidan Damian Mlawa amechukua rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania ubunge wa Jimbo la Kilolo katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiahidi kushirikiana na wananchi na serikali kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Mlawa amesema dhamira yake ni kuendelea kujitolea kuisaidia jamii kupitia nafasi ya kisiasa, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada zake binafsi alizozifanya kwa miaka mingi akiwa mdau huru wa maendeleo.
“Naingia kwenye mchakato huu nikiwa na nia njema, dhamira ya kweli na upendo wa dhati kwa wananchi wa Kilolo. Tunahitaji kasi zaidi ya maendeleo ili kuendana na dira ya taifa inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ameleta mageuzi makubwa nchini,” amesema.
Ameipongeza CCM kwa kuendeleza misingi ya demokrasia ndani ya chama kwa kuwaruhusu makada wake kuomba ridhaa ya kugombea, na akaeleza kuwa kwa sasa anasubiri hatua nyingine ya uteuzi.
Mlawa amesisitiza kuwa yuko tayari kuwa msaidizi thabiti wa Rais na serikali yake, akiahidi kuendeleza ushirikiano na wadau wote katika kuhakikisha Kilolo inanufaika na fursa zilizopo kitaifa kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.