Mnada mkubwa wa vitabu Afrika kufanyika Tanzania

Mnada mkubwa wa vitabu Afrika kufanyika Tanzania

KAMPUNI ya Big Bad Wolf imedhamiria kuleta mageuzi kwenye uuzaji wa vitabu ambapo inatarajia kufanya mnada mkubwa wa vitabu Afrika na Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kupata bahati hiyo.

Mnada huo utafanyika kuanzia Septemba 8 hadi 18 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo kutakuwa na zaidi ya nakala 500,000 za vitabu kutoka kwa waandishi wakubwa 15,000 wa mataifa mbalimbali duniani.

Tayari Big Bad Wolf wenye makao yao nchini Malaysia wamefanya minada 13 katika miji tofauti ikiwamo Cambodia, Hong Kong, Indonesia, Myanmar, Pakistan, Ufilipino, Sri Lanka, Korea Kusini, Singapore, Thailand, Taiwan, Falme za Kiarabu (UAE) na Afrika Tanzania itakuwa nchi ya kwanza.

Advertisement

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Big Bad Wolf, Andrew Yap, alisema dhamira yao ni kukuza mazoea ya usomaji wa vitabu na kujenga kizazi cha wasomaji, hivyo wameamua kuweka punguzo hadi la asilimia 80 ili kutoa fursa kwa Watanzania kujipatia vitabu.

Naye mwanzilishi mwenza wa Big Bad Wolf, Mohamed Noor, alisema vitabu vyao ni vile vilivyowekwa sokoni miaka ya karibuni na ni vitabu vya kimasomo vyenye maadili kwa watoto na hadithi na vimeandikwa na waandishi kutoka mataifa mbalimbali lakini akasema hakuna vitabu vilivyoandikwa na Watanzania.

“Kwa kuwa hii ni mara yetu ya kwanza kuuza vitabu nchini Tanzania hatutakuwa na vitabu vilivyoandikwa na Watanzania lakini tutakaporudi kwa mara ya pili tutatoa nafasi kwa waandishi wa Kitanzania kuuza vitabu vyao,” alisema.