Mollel: Bima ya afya kwa wote haitabagua ugonjwa

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameweka wazi kuwa, Bima ya Afya kwa wote ndio suluhu ya changamoto za magonjwa yote, kwani wananchi watatibiwa magonjwa yote ikiwemo ugonjwa wa Selimundu bila gharama kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali ya taifa.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Februari 10, 2023 wakati akijibu swali la nyongeza la Joseph  Kakunda katika Mkutano wa 10  kikao cha tisa, Bungeni Jijini Dodoma.

Amesema, licha ya Wizara ya Afya kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga katika mfuko wa bima ya afya, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali yake ya awamu ya  sita ameendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya matibabu ya magonjwa hayo.

Advertisement

Amesema,  tayari Sh Bilion 11.5  zimetolewa na Rais Dkt. Samia kupitia Serikali yake kwa ajili ya ununuzi wa kifaa chenye uwezo wa kupima vinasaba ili kutambua tatizo hilo na kulitibu.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, tayari Hospitali za Rufaa za Mikoa zimeanza kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya bima kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa seli mundu ili waweze kupata matibabu.