Moshi wapata meya mpya

KILIMANJARO: Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamemrejesha Diwani wa Kata ya Njoro, Mhandisi Zuberi Kidumo, katika nafasi ya Meya wa Manispaa hiyo baada ya kumpigia kura zote 28 za ushindi.
Uchaguzi huo umefanyika jana Desemba 5, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Moshi na kushuhudia umoja wa madiwani katika kumpa tena dhamana ya kuliongoza Baraza la Madiwani.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Meya Mhandisi Kidumo aliwashukuru madiwani kwa kumuamini na kumpa nafasi nyingine ya kuendelea kuongoza, akiahidi kuimarisha maendeleo, uwajibikaji na utendaji wenye tija katika Manispaa hiyo.
Alisema ushindi alioupata unaakisi mshikamano, umoja na nia ya pamoja ya kuwatumikia wananchi wa Moshi kwa uadilifu, ubunifu na kasi mpya katika kuisukuma mbele agenda ya maendeleo.
Katika nafasi ya Naibu Meya, madiwani wamemchagua Diwani wa Kata ya Longuo B, Benedict Mwashamba, ambaye pia aliungwa mkono na idadi kubwa ya kura, akipewa dhamana ya kusaidia uongozi huo mpya unaoanza.



