Moto wateketeza vibanda vya biashara Kigoma
VIBANDA 148 vya biashara katika soko la mitumba Selemala Manispaa ya Kigoma Ujiji vimeungua kufuatia kuzuka kwa moto mkubwa usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kigoma, Ispekta Jacob Chacha akizungumza eneo la tukio alisema kuwa walipokea taarifa ya moto huo saa nane usiku na ndipo walipofika eneo la tukio kwa ajili ya uokoaji.
Hata hivyo Chacha alisema kuwa walifika eneo la tukio moto ukiwa umeathiri sehemu kubwa ya vibanda vilivyokuwa vinaungua na hivyo kuanza kudhibiti maeneo ya jirani ambayo yalikuwa na hatari ya kuathirika na moto huo ili viweze kuokolewa na kwamba hakuna madhara kwa binadamu.
Chacha alisema kuwa baada ya kufika eneo la tukio walikuta moto ni mkubwa hivyo wakaomba msaada wa gari la zimamoto kutoka uwanja wa ndege wa Kigoma na gari la kubebea maji ili kupata urahisi wa kuwa na maji karibu.
Kamanda huyo wa zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma alisema kuwa eneo lililoathirika na moto ni Block J lililokuwa na vibanda 148 ambapo vibanda 111 vilivyoungua vilikuwa na biashara na vibanda 37 havikuwa na biashara.
Alisema kuwa katika eneo hilo kuanzia Block A hadi Block J kulikuwa na jumla ya vibanda 727 ambapo vibanda 377 ndiyo vilikuwa na biashara na hivyo kufanya jumla ya vibanda Zaidi ya 500 kuweza kuokolewa.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma.Filemon Makungu akizungumza na waandishi wa Habari eneo la tukio alisema kuwa moto huo umeanza majira ya saa saba usiku ambapo eneo lililoungua kulikuwa na jumla ya vibanda 148 ambapo vimebanda 111 vyenye biashara vimeungua na vibanda 37 havikuwa na biashara.
Kamanda Makungu alisema kuwa hadi sasa bado chanzo cha moto huo hakijajulikana na uchunguzi tayari umeanza kuhusu chanzo cha moto na kwamba kwa sasa hali ya ulinzi katika eneo hilo umeimarishwa ili kuzuia wizi katika vibanda ambavyo havijaathirika na moto huo.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo akiwemo Rashidi Mkayala ambaye anauza mitumba eneo hilo alisema kuwa wameshtushwa sana na moto huo na taarifa kwamba umeme ndiyo chanzo cha tukio hilo inaweza kuonekana ndiyo sawa lakini uchunguzi kamili ufanywe.
Alisema kuwa uungaji umeme katika vibanda vingi umekuwa wa kienyeji kwa vibanda Zaidi ya kimoja kuungwa kwa mita moja na upitishaji nyaya pia haujazingatia utaalam kwa ajiili ya masuala ya usalama.