Mpango aagiza mageuzi ufugaji samaki JKT

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lifanye mageuzi ya ufugaji wa samaki. Pia amewataka kuwekeza ipasanyo katika uzalishaji wa chakula cha samaki hatua ambayo itasaidia kuondoa changamoto ya uhaba wa chakula hicho na kuwa na bei nafuu.
Dk Mpango alisema hayo Dodoma alipokagua mabanda ya ufugaji wa samaki kwa njia ya kisasa ya kizimba na mabwawa.
Alisema JKT imekuwa ikifa ya vizuri katika sekta ya ufugaji wa samaki na kuitaka kuendelea kutoa elimu na Teknolojia kwa wananchi ili ushiriki wa wananchi katika kufuga samaki uwe mkubwa.
“Mimi naamini JKT inaweza kabisa kuwa chemchem ya kubadilisha ufugaji wa samaki katika taifa letu, tunahitaji sana lishe na samaki hawa ni lishe bora kweli kweli na hatuna sababu ya watoto wetu wakose virutubisho na tunauwezo wa kufuga hata kwenye mikoa ya Dodoma na Singida kwa sababu maji yanayotumika sio mengi,”alisema Dk Mpango.
Aliongeza: “Hivyo tangazeni shughuli mnazofanya na mpeleke elimu na utaalamu huu kwa wananchi ambao wanahitaji sana elimu. Hakuna chocte uagizwa kutoka nje katika kutengeneza mabwawa.” Aidha, Dk Mpango pia aliwataja JKT kushiriki katika kutatua tatizo la chakula cha samaki kwa kuwekeza kuzalisha.
“JKT mna wataalamu muwekeze sana kwenye hili la chakula cha samaki, hatuna sababu ya kuagiza chakula cha samaki kutoka nje, maana maharage ya soya yanapatikana, pumba za mahindi, dagaa, uduvi vyote vipo tunaweza kabisa kutengeneza chakula cha samaki ili iwe bei nafuu.”
Akiwa kwenye banda la kuzalisha bidhaa za ngozi maofisa wa JKT walibainisha kuwa changamoto iliyopo kwenye uzalishaji wa bidhaa za ngozi vikiwemo viatu ni upatikanaji na malighafi na wimbi la uongizaji wa bidhaa na viatu visivyo vya ngozi asilia kutoka nje ya nchi.
Aidha, Dk Mpango alitoa rai kwa JKT lizirejeshe kwenye kiwango cha juu shule wanazozimiliki kiwemo Shule ya Sekondari ya Jitegemee.