Mpango aagiza mifuko ya plastiki kukamatwa

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza kuanzwa kwa operesheni ya kukamata na kuzuia mifuko ya plastiki nchini, inayochangia kurudisha nyuma jitihada zinazofanywa na serikali za kuiondoa kwa kuwa inaharibu mazingira.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla wakati wa mkutano wa viongozi wa masoko uliohusu masuala ya usimamizi na udhibiti wa mifuko ya plastiki.

Makalla alisema Dk Mpango alitoa agizo hilo walipokutana jijini Dar es Salaam, alipozungumza naye kuhusu uchafuzi wa mazingira unaoendelea nchini kupitia mifuko ya plastiki.

Kutokana na agizo hilo, Makalla ameagiza kuanza mara moja kwa operesheni ya kukamata watengenezaji wa mifuko ya plastiki katika viwanda bubu jijini Dar es Salaam.

Pia ameagiza kuanzia Jumatatu ijayo kufanyike operesheni ya kukamata mifuko yote inayotumiwa katika masoko yote yaliyopo katika mkoa wake.

“Tupo hapa tukasimamie jambo hili kwa nguvu zetu zote. Mifuko hii ina madhara kiuchumi, kiafya na katika mazingira,” alisema.

Alisisitiza kuwa wale walioruhusiwa kuzalisha mifuko hiyo mbadala kutokana na kuwepo kwa utitiri wa mifuko ya plastiki hivi sasa wanafunga viwanda vyao.

Aliwataka viongozi wa masoko baada ya mkutano huo kwenda kuelimisha wafanyabiashara ili waache mara moja kununua, kusambaza na kuuza mifuko hiyo.

Katika utekelezaji wa kazi hiyo aliwataka maofisa masoko kutoa taarifa za kila siku kwa wakurugenzi kwa ajili ya kuripoti mwenendo wa mifuko hiyo ili soko likikutwa kuna mifuko hiyo aweze kuwajibishwa.

Alilitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutimiza wajibu wake kwa kutoa elimu kwa umma na tamko kuwa operesheni ya ukamataji wa mifuko hiyo ni kwa nchi nzima, si Dar es Salaam pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Samuel Gwamaka alikiri vifungashio vya plastiki kurudi kwa nguvu pamoja na jitihada kubwa wanazozifanya za kuvidhibiti kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna nchi hazijaweka zuio la mifuko ya plastiki hivyo inaingia nchini kupitia mipakani.

“Kwa hiyo tunapata changamoto nyingi Kanda ya Ziwa, mikoa ya Kaskazini, Kusini na Magharibi. Tatizo limezidi kuwa kubwa kwa kuwa vifungashio hivi vinavyoingia sokoni tunapambana na mifuko rahisi kwa gharama ndogo,” alisema.

Akizungumzia kuhusu tamko hilo, Mwenyekiti wa Soko la Tazara Vetenari, Daniel Mlangu alisema amelipokea agizo hilo na yuko tayari kwa ajili ya utekelezaji wake.

Naye Katibu Mkuu wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Masoud Chauka alikiri kurudi upya kwa mifuko hiyo kwa kupitia njia za panya hivyo akasema ni jukumu lao viongozi kuelimisha wafanya biashara wadogo kutokuitumia.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa Kampuni ya Al Haseeb Jenery Ltd, Fulgence Lwiza alisema wazalishaji mifuko mbadala wameathirika kwa kiwango kikubwa baada ya kuibuka upya kwa mifuko hiyo ya plastiki.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button