MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na mamlaka za serikali za mitaa waongeze nguvu kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
Dk Mpango ametoa maagizo hayo baada ya kuongoza kazi ya kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani jana.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2023 inasema: Shinda uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki.
“Hakikisheni mnachukua hatua za kisheria kwa wale wanaokiuka maagizo haya. Lakini pia watendaji wote wanaohusika wasimamie kwa karibu uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala,” alisema na kuongeza:
“Wahakikishe mifuko yote inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji, yaani anuani yake, mifuko inazalishwa wapi na kama mifuko hiyo inakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.”
Pia alisisitiza kampuni na watu binafsi wanaozalisha bidhaa za plastiki wahakikishe takataka zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa zinakusanywa na kuondolewa.
Dk Mpango aliagiza mamlaka za serikali za mitaa zihakikishe kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa takataka ziwe na uwezo kufanya kazi kwa ufanisi.
Alikemea utoaji wa zabuni za uzoaji takataka kwa kampuni zisizo na uwezo na zile zisizo na vitendea kazi vya kisasa na akaziagiza halmashauri ziweke miundombinu ya uhakika ya ukusanyaji na usombaji wa takataka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko kama sokoni, stendi na hospitalini.
Aidha, Dk Mpango alihimiza wananchi watambue wajibu wao katika kutunza vyanzo vya maji, waache mazoea ya kutupa takataka hovyo na akaagiza kila kaya iwe na sehemu mahususi ya kuhifadhi ama kuchomea takataka.
“Sio ustaarabu kila mahali kufanya ni jalala la kutupa taka, ni lazima sasa tujenge tabia ya kuyaweka mazingira yetu yawe safi…lakini ninawataka pia wamiliki wa mabasi na magari binafsi wawe na vyombo au vikapu vya kuweka taka katika magari yao,” alisema.
Alisema masuala ya kufanya usafi na utunzaji mazingira hayana mbadala kwa kuwa mazingira ni uhai na yana uhusiano wa moja kwa moja na ustawi wa taifa kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo alisema suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira limeendelea kupewa kipaumbele nchini na kwa kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kaulimbiu inahamasisha ajenda ya utunzaji wa mazingira na kutunza vyanzo vya maji.
Dk Jafo aliwapongeza wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwa kujitoa kuhifadhi mazingira ikiwamo kampeni ya soma na mti yenye lengo la kuhamasisha upandaji wa miti shuleni.