MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amehimiza Watanzania wapande miti na kuzingatia usafi kwa kuwa mvua hazitabiriki na zinanyesha wakati usiotarajiwa kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.
Dk Mpango amesema hayo wakati akiwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Petro iliyopo Swaswa jijini Dodoma jana baada ya kushiriki ibada ya Jumapili kanisani hapo.
“Kila familia mjitahidi kupanda walau miti mitatu. Mmoja wa kivuli, miwili ya matunda. Na matunda ya aina nyingi yanastawi hapa Dodoma kwetu. Lakini vile vile usafi wa mazingira yetu. Tusitupe takataka ovyo ovyo, tujitahidi sana. Nchi nzuri tuliyopewa na mwenyezi Mungu tuitunze, tusiharibuharibu” alisema.
Dk Mpango alizungumzia suala la maadili akasema nchi hivi sasa ipo kwenye mtihani na akasema anashani kuna mahali taifa limekosea.
Ameomba Watanzania wajitafakari kuhusu malezi ya watoto, wanawaongozaje nyumbani, shuleni na vyuoni.
“Wakristu na Watanzania wote kwa ujumla kweli tunatakiwa tuombe huruma ya Mungu, tumekosea. Malezi ya watoto, malezi ya vijana wetu nadhani tumeyaacha pembeni”alisema Dk Mpango.
Hivi karibuni alihimiza wazazi watoe miongozo ya malezi kwa vijana sanjari na kuwalinda watoto wa kiume.Dk Mpango alisema hayo Dodoma wakati yeye na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango walipoungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma katika ibada ya Jumapili ya Sikukuu ya Pasaka.
“Zamani tulikuwa tunasema nitafuga mbwa kuchunga watoto wangu wa kike, sasa zamu imefika tuchunge na watoto wa kiume, wanaharibiwa sana huko mitaani, Kristo mfufuka hataki haya,”alisema.
Dk Mpango aliwasihi wazazi na walezi wawalinde watoto na vijana dhidi ya matumizi mabaya ya simu na kufuatilia mienendo yao.
Aliwaasa wazazi na walezi walee watoto kwa kuzingatia maadili mema ya Kitanzania na kuwa makini na maudhui ya watoto (katuni) katika televisheni ili kuwaepusha na kujifunza mambo yasiyofaa.
“Wazazi wenzangu nawaomba sana muwe makini na watoto wetu wanaangalia nini, hayo makatuni huko kwenye luninga wanaonesha madudu…kwa hiyo tufuatilie sana maadili ya watoto wetu na maadili ya vijana wetu tusiwaache wenyewe,” alisema Dk Mpango.