MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango amewasihi Watanzania kutatua migogoro ndani ya familia kwa njia bora na sahihi zaidi ili kuepukana na athari zinazowakumba watoto ikiwemo kubaki yatima.
Alitoa wito huo jana mara baada kutembelea kituo cha watoto yatima cha Jerusalem Home of God’s Love For Children kinachohudumiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kimara mkoani Dar es salaam.
Kituo hicho kinahudumia watoto ambao hutelekezwa au kutupwa na wazazi wao kuanzia siku moja baada ya kuzaliwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Alisema ni muhimu kila Mtanzania kuguswa na kutambua ni kosa mbele ya Mwenyezi Mungu na jamii kutupa mtoto ambaye ni zawadi kutoka kwa Mungu.
Alitoa wito wa familia kujiepusha na ugomvi na migogoro na pale inapotokea basi yafaa kutumia njia bora za utatuzi kama vile dini, wazee na serikali.
Dk Mpango alizipongeza taasisi za dini nchini kwa kuendelea kujitoa kuhudumia watoto yatima na wale wanaopitia mazingira magumu na kuwashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuhubiri amani, kuombea viongozi wa nchi pamoja na kuliombea taifa.
Alitoa shukrani kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kimara, Dar es Salaam kwa fikra za kuhakikisha kituo hicho cha watoto yatima kinakuwa endelevu kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika elimu na huduma za afya na kituo cha malezi kwa wazee.
Aliongeza kuwa suala la kuanzisha kituo cha huduma za afya pamoja na hospitali kwa ajili ya kufundisha wataalamu wa afya katika eneo hilo litakuwa msaada kwa watoto yatima wanaolelewa hapo, jamii ya eneo hilo pamoja Watanzania kwa ujumla.
DK Mpango aliwapongeza kwa kupanda miti katika eneo la hekari zaidi ya 1500 kwa lengo la kuhifadhi mazingira na alitoa wito pia kwa Watanzania kuacha tabia ya uvamizi katika maeneo ya taasisi za dini.
Alisema pia ni muhimu kuhakikisha maeneo ya taasisi za dini yanapimwa mapema ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza na kuwahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuona ni wajibu wao kutunza nchi kwa kupanda miti na usafi wa mazingira kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.