Mpango kumuua mwanaharakati wa tembo ulivyosukwa

Wayne Lotter

AGOSTI 16, 2017 jiji la Dar es Salaam na dunia kwa ujumla lilipokea taarifa ya kusikitisha ya kifo cha Wayne Lotter, Mkurugenzi wa Taasisi ya Protected Area Management System (PAMS), inayojishughulisha na harakati za kupambana na ujangili chini ya mwamvuli wa utetezi na uhifadhi wa wanyama pori.

Lotter ambaye anatambulika Tanzania kama Mwanaharakati wa Tembo alikutwa na umauti baada ya kupigwa risasi karibu na eneo la makazi yake la Baobab Village, Masaki, Dar es Salaam alikokuwa anaishi. Siku ya tukio, Lotter na Mkurugenzi mwenza wa PAMS ambaye hakutajwa jina walikuwa wakitoka jijini Arusha katika harakati zao za kazi.

Walipofika karibu na eneo hilo walikutana na majambazi ambao waliwavamia na baadaye walimpiga risasi Lotter. Tukio hilo kama yalivyo matukio mengine ya uhalifu liliingiza Jeshi la Polisi katika uchunguzi ili kubaini wahusika wa tukio ambapo takribani watuhumiwa 22 walikamatwa kabla ya kuchujwa kwa sababu mbalimbali na kubaki 11 waliokwenda hadi mwisho walipohukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi kusikiliza shauri hilo chini ya Jaji Leyla Mgonya.

Advertisement

Washtakiwa hao ni Rahma Mwinyi, Nduimana Ogiste, Godfrey Salamba, Chambie Ally, Allan Mafue, Ismail Mohamed, Leonard Makoi, Ayoub Kiholi, Abuu Mkingie, Habonimana Nyandwi na Michael Kwavava. Ni katika hukumu hiyo ndipo maelezo ya wahusika wa mauaji hayo yanapobainisha mpango mzima ulivyofanyika mpaka kutekeleza mauaji ya mwanaharakati huyo.

Mpango ulianzia jijini Arusha kwa mshtakiwa wa nane, Leonard Makoi ambaye katika ushaihidi ndiye anaonekana kuratibu mpango mzima kuanzia mwanzo. Makoi kwenye maelezo ya onyo alieleza kushiriki kutafuta watu wa kutekeleza mpango huo kuanzia mwanzoni.

Alikaririwa akisema: “Ni kwamba, mwaka 2017 mwezi wa saba tarehe sikumbuki, alinipigia simu mzee mmoja anayeitwa Machips, jina kamili silifahamu (akimaanisha mshtakiwa wa saba, Ismail Mohamed). Akaniambia kuna biashara anataka aongee na mimi.

“Majira ya saa saba usiku nilienda tukakutana na Mzee Machips, akaniambia kuna kazi ya Dar es Salaam. Nilipomuuliza ni kazi gani akaniambia kuna Mzungu anayehusika na meno ya tembo anatakiwa auwawe. “Akaniambia kama kuna watu wanaweza kufanya hiyo kazi niongee nao, tukubaliane ili kazi ifanyike. Baada ya kuniambia hivyo nilimweleza kwamba kuna kijana anaitwa Karama anaweza akafanikisha hiyo kazi,” alieleza katika sehemu ya maelezo yake.

Kwa mujibu wa maelezo yake walikubaliana na Karama ambaye baada ya makubaliano alimpigia akimtaka amtumie fedha kwa ajili ya maandalizi ya kazi hiyo.

“Baadaye Karama alinipigia simu akaniambia nimtumie pesa Sh milioni tatu kwa ajili ya kununua bunduki ya kufanyia kazi. Niliwasiliana na Mzee Machips akanipa hiyo pesa nikaituma kwa njia ya basi la Kilimanjaro Express. “Mwezi wa nane tarehe sikumbuki mwaka 2017. Ile kazi ilikuwa imekaribia na Mzee Machipsi alinipa pesa Sh milioni 58, nikaenda nazo Dar es Salaam kwa ajili ya kuwalipa akina Karama na wenzake akiwemo Gody na Mrundi ambae simfahamu kwa jina. “Ile kazi ilifanyika yule Mzungu akauwawa. Baada ya kazi kesho yake nilimpigia Karama akaja maeneo ya Ubungo katika hoteli ya Blue Pearl, nikamkabidhi kibegi kikiwa na Sh milioni 52 na kiasi kilichobaki, Sh milioni 6 nikabaki nacho, nikarudi Arusha,” alieleza.

Karama ambaye hakuwa mmoja washtakiwa mahakamani aliendelea kutajwa katika maelezo ya washtakiwa wengine kwamba ndiye aliyeratibu mpango huo kwa asilimia kubwa ikiwa ni pamoja kutafuta silaha, kuwahifadhi na kufanya nao vikao vya kuratibu mpango huo nyumbani kwake.

Katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Nduimana Ogiste, raia wa Burundi, alieleza namna alivyowasiliana na Karama ambaye alimtaarifu kuhusu mpango wa mauaji uliopangwa kufanyika Dar es Salaam na kuthibitisha kuwa alitumiwa shilingi milioni tatu kwa ajili ya kununua silaha.

Yeye alikiri pia kupokelewa na Karama alipowasili Stendi ya mabasi Ubungo kutoka Burundi na kupelekwa kuishi nyumbani kwake (Karama) Temeke.

Alikiri pia kushiriki vikao mbalimali vilivyofanyika kwa Karama kwa lengo la kupanga na kutekeleza mauaji ya Lotter.

Agosti 16, 2017 Lotter na Mkurugenzi mwenza wa PAMS walikuwa wakisafiri kutoka Arusha kuelekea Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) bila kujua kuwa walikuwa katika mpango wa kuuawa kwani nyuma yao kulikuwa na mtu anayetoa taarifa za safari yao na mbele yao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kulikuwa na watu wanaowasubiri kutekeleza uharamia juu yao.

Kati yao walikuwa ni watu wanaowafahamu, yaani madereva wao wanaowatumia katika safari zao mara zote yaani Chambie Ally na Daudi Kwavava.

Chambie yeye alishiriki mpango huo kutokea Arusha ambapo alitoa taarifa ya kuondoka kwa Lotter Kiwanja cha Ndege wa Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kuelekea Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) na Kwavava alishiriki mpango huo kwa kwenda kuwapokea na kuhakikisha anarahisisha mazingira ya kutekeleza mauaji hayo.

Saa chache kabla ya kwenda JNIA kuwapokea Lotter na mwenzake, Kwavava kwa mujibu wa ushahidi inaelezwa kwamba alipitia dukani kwa mshtakiwa wa sita, Allan Mafue ambaye anatajwa kuwa alifadhili mpango huo wa mauaji na ndiye aliyemlipa Ogiste ujira wake wa Sh milioni 20 kutokana na kazi aliyofanya katika mpango huo.

Kwavava alienda kuonana na Mafue kwa ajili ya maelekezo ya mwisho ya utekelezaji wa mpango wao. Tukio hilo pia lilithibitishwa na Ogiste ambaye kwenye maelezo yake alieleza kuwa alimshuhudia Kwavava akiingia dukani kwa Mafue ambako alikaa kwa dakika thelathini kwa ajili ya kukamilisha mpango huo.

“Walikaa kama dakika thelathini au zaidi, baadaye walitoka na yule mzee aliondoka. Karama aliniambia, tuingie ndani ya gari. Tulipoingia alisema kazi ipo. Na yule mzee aliyekuwa naye (akimaanisha Kwavava) ndiye dereva atakayemchukua Mzungu uwanja wa ndege. Wameshaongea naye walipoingia ndani kwa Mafue, tuliondoka kwenda uwanja wa ndege.” Ushahidi ulionesha kwamba walipofika JNIA, Kwavava aliwapokea Lotter na mwenzake na safari ya kuelekea Masaki ilianza bila Lotter kujua kwamba nyuma yao Karama na Ogiste walikuwa wakiwafuatilia kwa kutumia gari aina ya Toyota IST kwa lengo la kuwaua.

Katikati yao dereva wa bodaboda, Ayoub Kiholi alikuwa akihakikisha usalama wa wauaji kwa kujiweka tayari kuwaokoa dhidi ya askari polisi na kuhakikisha hawavurugi mpango wao.

Awali katika maelezo yake, Kwavava alisema kuwa Agosti 16, 2017 akiwa amewabeba abiria wake kutoka JNIA, walifika katika makutano ya barabara ya Haile Sellassie ambako gari aina ya Toyota IST yenye paa jeusi iliwazuia kwa mbele na wakashuka watu wawili wenye silaha kuelekea kwenye gari yake.

Alisema mmoja wao alifyatua risasi na kumpiga Lotter karibu na kidevu huku akimwacha mwenzake ambaye ndiye aliyekuwa karibu zaidi.

Kwavava alitoa maelezo hayo kana kwamba alikuwa hajui chochote kuhusu mpango huo mpaka pale uchunguzi wa wa polisi ulipokuja kumbaini kwamba alishiriki na kumtia nguvuni.

Washtakiwa wengine kama Rahma wanaingia katika kesi hii kwa kushiriki njama za mauaji ambapo ushahidi ulionesha alishiriki kuwahifadhi na kuwaandalia chakula wahalifu walioshiriki mpango huo nyumbani kwa kaka yake Karama ambaye alikuwa akiishi naye huko Temeke Pia Rahma, kwa mujibu wa ushahidi alishiriki kuficha silaha zilizotumika kutekeleza mpango huo kwa kwenda kuzizika katika makaburi ya Ngazija Upanga, Dar es Salaam baada ya kusikia kuwa kaka yake alichukuliwa na watu wasiojulikana na yeye kuhisi kuwa amekamatwa na polisi.

Ingawa haikujitokeza waziwazi sababu ya kumuua Lotter, lakini inaaminika ni kutokana na harakati za kupambana na majangili.