Mpango majaribio wataalamu wa kujitolea wazinduliwa
DODOMA; SERIKALI imezindua mpango wa maiaribio wa wataalamu wa kujitolea kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Afya na Taasisi ya kimarekani ya US Peace Corps.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Grace Magembe amesema kuwa huo ni mpango wa majaribio na utahusisha vijana kutoka Tanzania na Marekani ukihusisha vijana wanaofanya kazi kwenye jamii.
“Mpango huu ulishaanza utekelezaji lakini vijana waliokuwepo walikuwa wakitoka Marekani tu, tuliona hii haijakaa vizuri, kwa nini vijana wetu hawapo tuliona wakikaa pamoja watajifunza mengi ikiwemo mila na desturi,” amesema na kuongeza kuwa hata walipozungumza na US Peace Corps walikubali mapendekezo ya serikali.
Magembe amesema kuwa taasisi hiyo ina watu 2,900 wanaofanya kazi mbalimbali za kujitolea na kwamba huduma za kujitolea hapa nchini zilianza tangu mwaka 1961, wakati wa uhuru mashirika yalishaanza kazi za kujitolea.
“Mradi huu ni wa majaribio ndoto ya serikali ni kuwa na miradi ya afya inayogusa sekta zote cha msingi ni kuzingatia yale yanayoelekezwa”amesema.
Amesema kuwa vijana huwa wabunifu huangalia mazingira na changamoto kisha hubadilisha kuwa fursa na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imejikita kutafuta fursa na kuwapa vijana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa US Peace Corps, Stephanie de Goes amesema kuwa mpango huo umeshirikisha vijana kutokana na kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi.
Amesema mradi huo unaanza kwa majaribio kwa mikoa miwili ya Dodoma na Iringa, ambapo vijana 26 watashiriki kazi za kujitolea. pamoja na wenzao kutoka nchini Marekani.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Kinga wizara ya Afya, Dk Tumaini Haonga amesema kuwa programu hiyo ni muendelezo wa huduma za kujitolea za nchini.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Paul Chawote, amesema kuwa mpango huo utasaidia kuongeza chachu ya uzalendo kwa vijana wa Tanzania na kuzitaka halmashauri za wilaya kishirikiana katika utekelesji wa mpango huo.
Meneja miradi wa US Peace Corps,Endesh Mollel amesema kuwa vijana 26 wakiwemo wa kike 13 na kiume 13 watashiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
“Vijana kutoka Wilaya ya Bahi na Chamwino mkoani Dodoma na Mufindi mkoani Iringa wenye elimu kuanzia ya diploma na digrii wamepata fursa ya kujitolea kwenye vijiji wanavyotoka,”alisema