DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wakandarasi wa usafi kuhakikisha wananunua na kutumia vifaa bora vya usafi ili kuboresha hali ya usafi jijini Dar es Salaam.
Mpogolo ameyasema hayo leo Februari 15, 2025 baada ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam linalofanyika kila Jumamosi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha Jiji la Dar es salaam linakuwa safi wakati wote.
“Tuna kasi kubwa ya kufanya Dar es Salaam iwe safi, na tunapaswa kuwa mfano kwa miji mingine, wezo tunao, nia tunayo, na lazima tuthibitishe hilo kwa vitendo,” amesema Mpogolo.
Soma zaidi: Mpogolo awapa neno maofisa usafirishaji
Aidha, amewashukuru wananchi na wadau wa mazingira kwa kushiriki katika zoezi la usafi na huku akimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabeya kwa kusimamia vyema usafi wa jiji na kuhakikisha Dengu beach inaakuwa safi na wa kuvutia.
Katika hatua nyingine, Mpogolo ametoa wito kwa mamlaka husika na wananchi kuhakikisha usafi unadumishwa kila siku, akisisitiza kuwa usafi wa jiji hautakiwi kuwa wa kampeni za mara kwa mara pekee.
Soma zaidi: Mpogolo: Tuzo ya Rais Samia imetuheshimisha
Naye, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amempongeza Mpogolo kwa juhudi ikiwemo za kusimamia usafi kila Jumamosi.
Mabeya amesema kuwa usafi ni utamaduni na tabia inayojengeka na kwamba wao kama halmashauri wapo tayari kutekeleza agizo la usafi kikamilifu.