Mradi SGR Makutopora – Tabora kukamilika 2028

TABORA: Utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha kutoka Makutopora – Tabora unatarajiwa kukamilika mwaka 2028 huku kazi za ujenzi zikiendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya mradi.

Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Christopher Kalisti anasema mradi huo unahusisha ujenzi wa kilomita 294 za njia kuu ya reli pamoja na kilomita 74 za njia za michepuko ambazo zitasaidia kuunganisha maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika eneo la Nyahua, leo Julai 19, 2026, Kalisti mradi huo utakuwa na vituo vya abiria na mizigo katika maeneo ya Manyoni na Itigi huku vituo vingine vikijengwa Goweko na Igalula Tabora.

Anaeleza kuwa kituo kikuu kitajengwa Tabora na kitakuwa kitovu cha kuunganisha reli zinazoelekea Mwanza na Kigoma.

Anabainisha kuwa reli hiyo itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya kati, kanda ya magharibi pamoja na nchi jirani hivyo kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri na biashara.

Kalisti anasema mkandarasi anaendelea na kazi kwa mujibu wa ratiba na mradi unatarajiwa kuingia hatua za ukamilishaji ifikapo mwishoni mwa mwaka 2028.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, anasema kukamilika kwake kutapunguza kwa kiasi kikubwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam, Dodoma na Tabora, huku reli ikiwa na uwezo wa kubeba tani 35 kwa kila ekseli, hali itakayopunguza gharama za usafirishaji wa mizigo.

Kwa upande wake Mhandisi upande wa Mkandarasi kutoka kampuni ya Yapi Markezi, Pangapanga Msisili anasema utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kiwango kinachoridhisha na haujawahi kusimama tangu ulipoanza.

“Sisi tunaona mradi wetu unaenda vizuri na jinsi mnavyoona.Tumejipanga kuhakikisha tunafuata ratiba ya mradi ili ukamilike kwa wakati ili reli hiyo iweze kuanza kutoa huduma kwa wakati na kuchangia kufanikisha malengo ya serikali ya kuboresha sekta ya usafiri na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa,”anasema Msisili.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button