Mradi wa bil 185/- kuwatua ndoo Morogoro (logo ya Kimkakati)

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) imeanza kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 185 kwenye Manispaa ya Morogoro.

Fedha hizo zinatokana na ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kuboresha Bwawa la Mindu na miundombinu ukiwemo ujenzi wa mtambo wa kutibu maji eneo la Mafiga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa, Tamimu Katakweba alisema hayo mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka huu, Sahil Geraruma.

Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi kwenye mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa mitaa ya Kasanga na Mgaza ambao idadi yao imeongezeka kutoka 3,918 mwaka 2014 na sasa kukadiriwa kufikia wakazi 10,000.

Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 umeweka kipaumbele katika upatikanaji na usambazaji wa majisafi na salama vijijini na mijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeielekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mijini inakuwa asilimia 95 na vijijini inakuwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Mhandisi Katakweba alisema mradi huo wa kimkakati unatarajia kukamilika mwaka 2025 ambao utazalisha maji lita milioni 89 ukilinganisha na mahitaji ya lita 86 kwa siku mwaka 2025.

Alisema utaboresha bwawa la Mindu kwa kunyanyua kuta na kuondoa tope, ujenzi wa mtambo mpya wa kutibu maji utakaojengwa eneo la Mafiga, ujenzi wa mabirika ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 11 kwa wakati mmoja na utafutaji wa vyanzo vya maji mbadala ukiwemo maji ya chini ya ardhi.

Katakweba alisema kwa sasa mahitaji ya maji kwa Manispaa hiyo ni lita milioni 73 kwa siku ukilinganisha na lita milioni 35 zinazozalishwa kwa sasa.

Mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji Kasanga ulibuniwa na Manispaa ya Morogoro mwaka 2014 ulikuwa na lengo la kuhudumia wakazi 3,918 wa mtaa wa Kasanga na Mgaza na ulikabidhiwa kwa mamlaka 2017 kwa ajili ya uendeshaji.

Katakweba alisema mradi huo ulitekelezwa na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Covid -19, Sh milioni 590.9 zilitolewa na serikali wakati Sh milioni 25.3 zilizotolewa na Moruwasa zilitumika kuboresha mradi huo kwa ajili ya wananchi wa mitaa ya Kasanga na Mgaza.

Alisema mradi huo baada ya maboresho makubwa utapunguza tatizo la mgao wa maji kwa wananchi wa Kata ya Mindu kutoka siku 14 za awali na sasa watapata maji kila baada ya siku moja kwa kuwa utakuwa na uwezo wa kusambaza maji lita 700,000 kwa siku huku mahitaji yakiwa ni lita 941,500.

Katakweba alisema serikali kupitia Mamlaka hiyo imekalisha miradi ya maji ya matokeo ya haraka kwenye maeneo ya Bigwa-Bohmela, Mambogo-Kihonda, Mkundi – Lukobe, Mindu, Mgadu, Kauzeni na Bong’ola na itaongeza lita milioni 17 kwenye mfumo hivyo kuongeza uzalishaji toka asilimia 48 za sasa na kufikia asilimia 71 kufikia Juni 2023.

Geraruma aliwataka wananchi wasilime na wasifuge kwenye vyanzo vya maji na wavitunze.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa ofisi ya mbunge katika kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapata huduma ya maji safi na salama.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button