Mradi wa maji Makongo-Bagamoyo wafikia patamu

Mradi wa maji Makongo-Bagamoyo wafikia patamu

MRADI wa maji wa Makongo hadi Bagamoyo, umefikia asilimia 87 kukamilika kwake, ukiwa unagharimu Sh bilioni 65.4.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Miradi ya Dawasa, Mhandisi Ramadhani Mtindasi, amesema mradi huo utakamilika Desemba na utaweza kuhudumia wananchi zaidi ya milioni moja.

Advertisement

 

Kukamilika kwa mradi huo ni neema kwa wakazi wa Makongo, Goba, Tegeta, Mbweni, hadi Mapinga wilayani Bagamoyo.

 

Mtindasi akizungumza leo katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam, amesema mradi huo una matenki  matatu ya maji yaliyopo Vikawe, Mbweni na Tegeta A.

 

Amesema mradi huo ambao umeanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ukiwa na kilomita 1250,  unatekelezwa kupitia wafadhili wa maendeleo chini ya usimamizi wa Dawasa kupitia Mkandarasi wa Kampuni ya  CDEIC  & HAINAN JOINT VENTURE .

 

“ Ujenzi wa matanki matatu makubwa ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni tano, pamoja na ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji vinavyojengwa eneo la Vikawe na Mbweni, ”amesema.  

 

Mtindasi amesema mradi huo utakapokamilika wateja 60,000 wa maeneo mbali mbali ya Changanyikeni, Vikawe, Goba, Mivumoni, Mbweni, Madale, Tegeta A, Bunju, Wazo, Ocean Bay, Salasala na Bagamoyo watanufaika.

 

Kwa upande wa Bagamoyo mradi utahudumia wakazi wa Kata za Mataya, Sanzale, Migude, Ukuni, Mtambani, Nianjema, Kimara Ng’ombe na Vikawe Bondeni.

 

Kwa upande wa Mabwepande mradi utahudumia kata ya Mapinga,  Salasala, Goba, Kinzudi, Mbezi na Kilongawima.

 

Mtindasi amesema lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kufikia asilimia 95 ya usambazaji maji kwa upande wa mjini na asilimia 85 kwa upande wa vijijini, lakini wao Dawasa wanatarajia kufikia asilimia 95 kabla ya 2025 na asilimia 100 ifikapo mwaka huo.

 

Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Adam Ngalawa, amesema wameridhika na utekelezaji wa mradi na kuitaka Dawasa kuongeza kasi, ili miradi ikamilike kwa wakati.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Godwin Gondwe akizungumzia mradi huo, aliwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa, kwani iwapo itahujumiwa watakaoathirika ni wao.

 

Kwa upande wa mkazi wa Mabwepande, Saida Gerald Lusato ameishukuru serikali kuwafikishia huduma ya maji, ambayo eneo hilo walikuwa na changamoto kubwa ya maji takribani miaka 10.