KAGERA; Mradi wa maji Byeju wilayani Missenyi mkoani Kagera wenye thamani ya Sh bilioni 2.4, ambao unatarajia kunufaisha zaidi ya wananchi 26,000 umefikia utekelezaji wa asilimia 90.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava ameipongeza Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kuendelea kukamilisha mradi huo utakaosadia wananchi wa vijiji vya Ngando, Byeju na Nkerenge.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto ya maji inayowakabili wananchi kwa muda mrefu na kusababisha baadhi ya shughuli nyingine zisifanyike kwa wakati.
Meneja wa RUWASA wilayani Missenyi Andrew Kilembe, akisoma taaarifa ya mradi huo amesema kuwa mkataba wa mradi ulisainiwa Octoba, 2023 na mkandarasi alianza kutekeleza mradi huo Desemba 2023 na unatarajia kukamilika hivi karibuni.
Soma pia: Wananchi kunufaika na mradi wa maji Biharamulo
“Mpaka sasa hivi kazi kubwa na muhimu zimekamilika , wananchi wengi wataaanza kupata maji ya uhakika baada ya kukamilisha mambo madogo yaliyobaki, tunaendelea kuishukuru serikali kwa kuleta pesa za mradi wa maji na kuwaondolea adha wananchi ambao wanatumia muda mwingi kufuata maji umbali mrefu na kushindwa kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi,”anasema Kilembe.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo La Nkenge, Frolent Kyombo ameishukuru serikali kwa mradi huo na mingine ya kimaendeleo wilayani humo.
Comments are closed.