WANANCHI zaidi ya 4500 wa kijiji cha Kasato kata ya Nyakanazi Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera wameondokana na shida ya upatikanaji wa maji baada ya mradi wa usambazaji maji chini ya Wakala wa Usambazaji wa Maji Vijijini – Ruwasa kukamilika.
Akisoma taarifa ya Mradi huo Mhandisi wa Ruwasa, Lucas Matina amesema mradi huo uliogharimu Sh milioni 316 umekamilika kwa asilimia 100 kwa miezi sita.
“Mradi wa maji Kasato uliohusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa Lita 50,000 umejengwa ndani ya miezi sita na umekamilika kwa asilimia 100 na unahudumia wakazi takribani 4500,”Matina amesema.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Eliakimu Mnzava akikagua mradi huo amesema wamejiridhisha kazi imefanyika vizuri na kumshukuru mwananchi Boniphace Matiba kwa kujitolea eneo bure la ujenzi wa tanki la maji.
“Tumejiridhisha kazi imefanyika vizuri Mwenge wa Uhuru utazindua mradi huu, pia tunamshukuru mzee Boniphace Matiba kwa kuona haja ya kutoa eneo lake ili kichimbwe kisima kama chanzo cha maji,” Boniface ameongeza.
SOMA: Mwenge wa Uhuru wakagua miradi ya Sh Bil 5 Iramba
Mbunge wa Biharamulo, Ezra Chiwelesa ameishukuru serikali kwa kusogeza huduma hiyo kwa wananchi kwani walikuwa wakipata shida ya maji na kuomba miradi mingine ya huduma za maji kusogezwa kwenye vijijini vingine kwani bado kuna uhitaji wa huduma hiyo.
“Huku ni mlimani kabisa hatukuwa na chanzo cha maji kwahiyo unaweza kuona sio kazi ndogo lakini pia licha ya kukamilika mradi huu kwa kiwango kizuri bado tuna uhitaji wa miradi mingine ya Maji,” amesema Chiwelesa.
Wananchi wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa maji kwani awali walikuwa wakitumia umbali mrefu kupata maji ambayo pia sio safi na salama.