Mradi wa maji wa bil 1.5/-Iringa una kasoro

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa imebaini kasoro kubwa katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Sadani-Kihata, wenye thamani ya Sh bilioni 1.5, unaofadhiliwa na Mfuko wa Maji wa Taifa.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Domina Mukama amesema ukaguzi uliofanywa Desemba 2024 katika Kata ya Sadani, wilayani Mufindi ulibaini changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa katika vijiji vitano vinavyonufaika na mradi huo wa maji.

Alisema uchunguzi ulibaini kuwa mabomba yaliyounganishwa kwa watumiaji wa majumbani yalipasuka, tatizo lilitokana na matumizi ya mabomba ya Daraja B badala ya Daraja C – ambayo ni kinyume cha miongozo ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA).

Advertisement

Aidha alisema mradi huo ulikosa uthabiti katika usakinishaji – kwa mabomba kutokazwa ipasavyo, hali iliyosababisha uvujaji mkubwa wa maji.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mukama alisema mradi huo, ambao tayari umetekelezwa kwa asilimia 90 na mkandarasi M/S Bejan Business Enterprises, umekwishatumia Sh Bilioni 1.067, sawa na asilimia 71 ya fedha za mradi.

Muhimu zaidi, Mukama alifafanua kuwa kosa hilo halikufanywa na mkandarasi huyo, bali lilitokana na msimamizi wa mradi kutoka chombo cha watumiaji maji ngazi ya jamii (CBWSO).

Mbali na kasoro katika mradi huo, alisema TAKUKURU pia ilifanya ufuatiliaji wa miradi yenye thamani ya Sh Bilioni 16.064, ambapo miradi mitatu ya sekta za maji, afya na elimu yenye thamani ya Sh Bilioni 1.23 ilibainika kuwa na changamoto.

Alisema ujenzi wa jengo la wodi ya wajawazito (Maternity Complex) – Mafinga wenye thamani ya Sh Milioni 500 ulikumbwa na kasoro ya mafundi kukosea kuweka marumaru katika baadhi ya sehemu za jengo.

Hata hivyo, baada ya ushauri wa TAKUKURU, maboresho yalifanyika na sasa ujenzi upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Na katika ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Ugwachanya, Mukama alisema mradi huo wenye thamani ya Sh Milioni 583, ilibainika kuwepo kwa vifaa vilivyotumika kutokuwa na vipimo vinavyoendana na mkataba, jambo lililokiuka Sheria ya Ununuzi ya Mwaka 2023 pamoja na Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2024.

Alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha kasoro zilizobainika zinarekebishwa na miradi yote inakamilika kwa viwango vinavyokubalika.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha za umma, huku ikitoa elimu kwa wananchi na taasisi mbalimbali juu ya madhara ya rushwa.

“Wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya rushwa katika miradi ya maendeleo. Tunawahimiza wote kushirikiana nasi kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya jamii,” alisema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *