WAKAZI wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wataondokana na changamoto ya uhaba wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi wa Sh bilioni 2.5 ambapo kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 65.
Akizungumza leo Novemba 5, 2024 katika ziara yake wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian ameishukuru serikali kwa kutatua changamoto ya maji.
Amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa bwawa la maji Kwenkambala kutasaidia wilaya hiyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma ya maji.
“Niwaombe wasimamizi wa mradi huu wahakikishe unamalizika kwa wakati lakini unakuwa na viwango bora Ili thamani ya fedha ambayo imetolewa iweze kuendana,”amesema RC Buriani.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando, mradi huo ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 65 huku ukiwa tayari umetumia kiasi cha Sh bilioni 1.5 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwaka huu.