Mradi wa umeme Kishapu kuanza na Megawati 50

KAIMU Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Elias Turnbull amesema mradi wa umeme wa jua uliopo wilayani Kishapu utaanza usambazaji wa Megawati 50.

Mhandisi Turnbull aliyasema hayo kwenye mdahalo wa wadau wa maendeleo waliokuwa wakijadiliana kuhusu nishati ya umeme ambapo walidai masaa ya kukatika kwa nishati hiyo yapungue ili kufanya shughuli zao na kuepusha mitaji kupotea na kuingia kwenye umasikini.

Mhandisi Turnbull alisema serikali ipo kwenye mikakati ya kuhakikisha kunakuwa na unapatikanaji umeme wa kutosha.

“Mkoa huu unamatumizi ya Megawati 70 mpaka sasa tukiongeza na hizi zitakazo zalishwa na Umeme jua tutakuwa na Umeme wa uhakika.”alisema Mhandisi Turnbull.

Alisema vyanzo vyote vya nishati ya Umeme serikali inavitambua na Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza suala la utunzaji wa mazingira misitu isikatwe hovyo kulinda vyanzo vya maji.

Mdau wa Maendeleo kutoka mkoani hapa mchungaji Meshaki Kulwa alisema mgawo wa umeme miezi yake inajulikana hasa kipindi cha kiangazi ushauri serikali iweke mikakati yakutosha kuhakikisha miezi hiyo haina mgawo wa Umeme na watu wanafanya shughuli zao.

Mwenyekiti wa chama Cha wafanyabiashara,Viwanda na kilimo (TCCIA) mkoa wa Shinyanga Jonathan Manyama alisema wao wamebeba maono ya wanachama kuhakikisha wanapata huduma nzuri kutoka serikalini na wao kulipa kodi bila usumbufu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Baadhi ya wafanyabiashara Shabani Kambo na Warioba Nassor waliohudhuria mdahalo huo walisema hotuba ya Rais waliisikia kutoa miezi sita kwa shirika hilo wajipange ili umeme uwepo wa uhakika hilo walilipongeza nakumtaka kuendelea kuwawajibisha wanaohujumu miundombinu.

Habari Zifananazo

Back to top button