Msako waanza wanaotelekeza watoto

Msako waanza wanaotelekeza watoto

HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga imeanza msako wa wazazi wa wanaotelekeza watoto.

Hatua hiyo imekuja baada ya uwepo wa viashiria vya ongezeko la mashauri ya wazazi kutelekeza watoto, katika kituo cha  msaada wa  sheria mkoani Shinyanga (PACESHI).

Mratibu wa Kituo hicho, John Shija,aliliambia HabariLEO kwamba jumla ya mashauri 170 yanayohusisha watoto 396  wa umri kati ya miaka miwili hadi saba, waliotelekezwa katika halmashauri hiyo yalipokelewa ndani ya kipindi cha Januari hadi Disemba, mwaka jana.

Advertisement

Shija amesema  uchunguzi wa awali umeonesha sababu kubwa ya tatizo hilo ni wanaume kuzaa nje ya ndoa, bila uwezo wa kuhudumia familia mbili.

“Wengine wamezaliwa ndani ya ndoa lakini migogoro ya kifamilia inawatenganisha wazazi. Watoto wanabaki kwa mama lakini baba hawajibiki kuwatunza,” alisema.

Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kituo kilipokea mashauri  11 yanayohusisha watoto 26, wa rika lile lile, waliotelekezwa, aliongeza.

Wakati huo huo,Shija alihimiza akina mama wawe na matumizi bora kwa watoto hao, kwani baadhi ya wanaume wamekua wakipeleka malalamiko kituoni hapo ya kutoa matunzo lakini hayawanufaishi walengwa ipasavyo.

“Matokeo yake akina baba wanaomba wawachukue watoto wao kuwatunza wenyewe, ili wawe na makuzi yanayostahili” alisema.

Alisema  sheria ya mtoto ya mwaka 2009, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, inaeleza kwamba wazazi wakitengana, mtoto anaweza kuishi na mama yake mpaka afikishe umri wa miaka saba lakini apate matunzo ya wazazi wake.

Ofisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Kulian Mlalama, alisema zipo pia familia ambazo wazazi wote wanatelekeza watoto kwa wanandugu, hivyo kufanya malezi na makuzi yao kuwa duni.

Alisema kwa upande mwingine mila na desturi za wasukuma zinachangia watoto kutelekezwa, pale ambapo wazazi wanatengana na baba kutaka kuishi na watoto wake kwa kigezo kwamba alitoa kiwango kikubwa cha mahari, wakati muda wa kuwaangalia hana.

Ofisa Ustawi alisema kwa sasa wanasakwa wanandoa waliotelekeza watoto watano katika  kitongoji  cha Mwabuluki,  kijiji cha Ng’wangosha, kata ya Nyamalogo, tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

“Tunaomba ushirikiano wa wanajamii wote, kwa sababu ulinzi wa  mtoto ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisema.