Msanii Eze Nice aleta tumaini kwa watoto yatima

MSANII wa kizazi kipya, Eze Nice, emewashika mkono watoto walio katika mazingira magumu wa kituo cha Amani Centre baada ya kuguswa na hali zao.
Tofauti na watoto wengine wanaopata nafasi ya kukutana na wasanii maarufu, Eze Nice amesema watoto hao wanahitaji msaada wa msingi wa maisha na wanahitaji pia burudani.
Kwa kuonesha dhamira ya kuwasaidia, Eze Nice alimfikia mfanyabiashara mkubwa wa mjini Iringa, Salim Asas, na kumpatia wazo la kusaidia kituo hicho.

Asas, anayefahamika kwa mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya jamii, hakusita kufanya hivyo katika tukio ambalo limekwenda na kusheherekea siku yake ya kuzaliwa.
Alisema Asas ametoa msaada wa vitu mbalimbali kituoni hapa unaojumuisha vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia, maziwa ya Asas, mafuta ya kupikia, sukari, vyakula na taulo za kike.
“Kama huwezi kuwasaidia watu, basi usiwaumize,” alisema Eze Nice wakati akielezea jinsi Asas anavyoshughulikia changamoto za makundi mbalimbali ya jamii mkoani Iringa.
Awali msimamizi wa kituo hicho, Elizabeth Mwakabanga, alisema kilianzishwa mwaka 2009 kwa msaada wa watu wa Ujerumani.
Alisema kituo hicho kilianza na watoto 13 na mabweni mawili, lakini sasa kina watoto 82 ambao kati yao wasichana ni 43.

Alisema kituo kinahifadhi watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu, kikiwapatia elimu, hifadhi, na msaada wa kisheria.
Hata hivyo alisema, kituo kinakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo upungufu wa mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi, vifaa vya shule, na vifaa vya michezo.
Mwakilishi wa Asas katika shughuli hiyo, Slavatory Ngelela alisisitiza mchango wa Asas kwa jamii akisema: “Hakuna mahali utakwenda Iringa usisikie msaada wa Asas. Tumempa tuzo ya maendeleo ya vijana.”
Wengine waliungana na Eze Nice kusaidia kituo hicho ni pamoja na Dj Nasi, aliyetoa ahadi ya kuhakikisha anawahamasisha wadau mbalimbali kushughulia changamoto zingine zinazokikabili kituo hicho huku nmmfanyabiashara Fred Vunja Bei, akiahidi kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo.
Watoto wa Amani Centre walifurahia si tu msaada huo, bali pia uwepo wa watu waliowaonesha kuwa wao ni sehemu muhimu ya jamii.



