MSD yaimarisha usafishaji damu, gharama kupungua

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai.

BOHARI ya Dawa Tanzania (MSD) imesema gharama za kusafi sha damu zitapungua kutoka kati ya Sh 200,000 hadi 230,000 kuwa chini ya Sh 100,000 kwa mzunguko mmoja baada ya kupatikana kwa wasambazaji watakaotoa huduma ya vifaatiba na dawa kwa wagonjwa wa fi go.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Tukai alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa uboreshaji wa MSD katika utoaji wa huduma zake na kuwa bila kuathiri ubora wa huduma hizo, bei ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo nchini wanaotibiwa kwenye hospitali za mikoa zitapungua.

Advertisement

Aidha, alisema mbali na matarajio hayo, serikali imeboresha huduma za afya nchini kuwa kujenga na kuboresha vituo vya kutolea huduma za tiba na sasa matibabu ya figo yameongezeka katika hospitali za mikoa.

Alisema MSD ilianza kutekeleza mradi wa kusambaza mashine za kusafisha damu katika hospitali za mikoa mwaka 2021/2022 na hadi kufika mwishoni mwa mwaka jana MSD ilikuwa imenunua mashine 137 za kusafisha damu.

“Idadi hiyo inaongeza mashine za awali 60 ambazo tayari tulishazisambaza kwenye hospitali hizo za mikoa zinazofanya huduma hiyo, lakini pia idadi ya hospitali zinazotoa huduma zimeongezeka kutoka sita za mwanzo hadi 15, Februari mwaka huu,” alifafanua Tukai.

Alisema uwekezaji huo umegharimu Sh bilioni 7.7 na lengo lake ni kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za kusafirisha damu karibu na maeneo yao hivyo kupunguza gharama zilizokuwa zikitumika awali kuifuata huduma hiyo mbali.

Akifafanua kuhusu kupungua kwa gharama za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, Tukai alisema kwa mwaka huu MSD wamepata wasambazaji watakaoshusha gharama za kusafisha damu kwa mzunguko mmoja.

“Tumezoea gharama za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo ni kati ya Shilingi 200,000 hadi 230,000 kwa mzunguko mmoja, kwa wasambazaji hawa gharama zitaenda kuwa chini ya Shilingi 100,000 kwa mzunguko na unafuu huo hautaathiri ubora wa huduma,” alisema bosi huyo wa MSD.

Alisema mkakati huo unatekelezwa chini ya uratibu imara wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na hospitali zinazotoa huduma za ‘hemodialysis’ ambapo kifurushi cha msingi cha vifaa vinavyotumika katika ‘hemodialysis’ kwa ajili ya vipindi 100.

Kuhusu mashine hizo 137 za kusafisha damu, alisema zimefungwa katika hospitali 11 za mikoa zilizoanza kutoa huduma hiyo na hospitali nne ziko hatua ya matengenezo.

Baadhi ya hospitali hizo za mikoa zinazotoa huduma hiyo ya kusafisha figo ni hospitali za rufaa za mikoa za Amana, Mwananyamala, Temeke, Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Sekou Toure na Benjamin Mkapa.

Akizungumzia upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya, Tukai alisema uwepo wa bidhaa za afya umekuwa ukipimwa kwa bidhaa za afya ashiria 290.

Hata hivyo, kuimarishwa mifumo ya utoaji huduma na nia ya serikali kuboresha maisha ya Watanzania, kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024, idadi ya bidhaa ashiria zinazotumika kupima hali ya upimaji wa bidhaa za afya zimeongezeka kutoka bidhaa 290 hadi bidhaa 382.

Tukai alisema katika hilo upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka na unaimarika mwaka hadi mwaka.

Alisema vituo vya huduma 8,466 vinahudumiwa na MSD kwenye huduma ya bidhaa za afya, na kiwango hicho imeongezeka kutoka vituo 7,095 mwaka 2021/2022.

Akizungumzia mapato ya MSD, alisema maboresho yanayoendelea na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali, umeongeza mapato ya taasisi hiyo kutoka Sh bilioni 315.1 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Sh bilioni 553.1 mwaka 2024.

Aidha, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025, MSD imepata mapato ya thamani ya Sh bilioni 400.2 sawa na asilimia 115 ya lengo la kusambaza bidhaa za afya zenye thamani ya Sh bilioni 346.6.

Kuhusu MSD kusambaza dawa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tukai alisema kulikuwa na changamoto za kimfumo katika nchi hizo 16 za SADC ambapo kila nchi ina utaratibu wake wa mfumo wa kuagiza dawa hivyo iliwalazimu kupitia upya suala hilo ili kuweka utaratibu mzuri.

“Kwa sasa jambo hilo limeanza upya na hata jana (juzi) baadhi ya wataalamu wetu wametoka Zimbabwe kuhusu suala hilo,” alisema Tukai.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *