Msumbiji kuleta wataalamu kujifunza JKCI, Muhimbili

DAR ES SALAAM: MKE wa Rais wa Msumbiji ,Gueta Selemane Chapo amesema nchi ya Msumbiji itashirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili nchi hiyo iwe inatoa huduma za moyo na upandikizaji mimba(IVF).

Akizungumza wakati wa ziara yake aliyoifanya katika taasisi ya JKCI amesema hospitali ya moyo inauwezo mkubwa wa kuhudumia wagonjwa wa nje 2,000 na wanaweza kulaza wagonjwa 100.

“Hospitali ya maputo haiwezi kufanya haya yote tunatamani ije ishirikiane na hizi hospitali kwa huduma za kibingwa tunatamani hospitali za namna hii kwenye nchi yetu katika ukanda wa kusini,kati na kaskazini ili iweze kuwahudumia mama zetu na dada zetu,”ameeleza.

Aidha amesema wameona namna wanawake wasioweza kuzaa wanavyosaidiwa hivyo wameweza kujifunza mengi wanatamani wanawake wa nchi yake kupata huduma hizo.

“Tunategemea kutuma ujumbe wetu kuja kujifunza ,tunashukuru sana kwa kuja Tanzania tumejifunza mengi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk Peter Kisenge amesema kikubwa alichokuja kuona ni teknolojia ambayo ipo ya kisasa ya kuwafatilia wagonjwa wanapofanyiwa upasuaji wakiwa nyumbani kwa kuwekewa shuka maalum.

Amebainisha kuwa kupitia shuka hiyo wanaona mapigio yao ya moyo,presha, upumuaji na mambo mbalimbali kuepusha vifo vya ghafla.

“Ameona watoto waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na taasisi kwa mwaka inafanya upasuaji wagonjwa 1,000 kwa mwaka na hii ni namba kubwa kwa njia ya tundu dogo wagonjwa 3,000 kwa mwaka na hii ni namba kubwa na sisi ndio wa kwanza Afrika.

Dk Kisenge amesema Msumbiji imeahidi kuendelea kushirikiana nao kwa kuleta wagonjwa na kuleta wataalam wao kuja kujifunza na hiyo ni sehemu ya tiba utalii.

Mkurugenzi wa huduma za tiba,Wizara ya afya Dk Hamad Nyembea amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza huduma zinazotolewa katika hospitali kubwa na Msumbiji wanakuja kujifunza kuona maendeleo makubwa katika huduma za kibobezi.

“Wamefurahi kuona tumesonga mbele kwenye huduma za kinamama,huduma za upasuaji wa moyo na huduma za watoto wadogo kwa ujumla amefurahia sana amejifunza ameona jinsi serikali inavyowajali wananchi wake na kuweza kuboresha huduma hizi ili wafaidike.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button