Msumbiji wajifunza nchini usimamizi mawasiliano

Msumbiji wajifunza nchini usimamizi mawasiliano

MENEJIMENTI ya mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini Msumbiji imefika Dar es Salaam kujifunza masuala ya usimamizi wa mawasiliano katika maeneo ambayo Tanzania imepiga hatua.

Maeneo hayo ni pamoja na usimamizi wa masafa, ubora wa huduma na mawasiliano katika maeneo ya mipaka.

Ujumbe huo kutoka Msumbiji ulipokewa juzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, John Daffa ambaye aliwapa maelezo juu ya kazi za TCRA.

Advertisement

Alifafanua dhamira ya TCRA kushirikiana nao katika kuwapa uzoefu wa mamlaka utakaowezesha usimamizi thabiti wa huduma za mawasiliano nchini mwao.

“Tuna uhakika ushirikiano huu ni muhimu katika kukuza sekta za mawasiliano kwenye nchi zetu na bila shaka wataalamu wetu watawapatia uzoefu mzuri wa namna sekta pana ya mawasiliano inavyosimamiwa hapa Tanzania,” alisisitiza.

Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Msumbiji, Francisco Chate alisema wana matumaini makubwa na uzoefu ilio nao TCRA katika kusimamia teknolojia na huduma za mawasiliano katika ukanda wa Afrika, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Lengo letu ni kuhakikisha nchi yetu inaunganishwa vilivyo na mtandao wa mawasiliano na ndio sababu ya ujio wetu Tanzania, tukiamini TCRA mnao uzoefu wa kutosha kutupatia maarifa zaidi ya namna tunavyoweza kusimamia na kuboresha huduma za mawasiliano hasa simu na intaneti,” alisisitiza.

Hii ni ziara ya pili kufanywa na mamlaka hiyo kwa TCRA ikinuia kufanya mageuzi makubwa ya namna inavyosimamia huduma za mawasiliano nchini humo hususani kuboresha ubora wa huduma na usambazaji wa huduma za mawasiliano katika majimbo ya Msumbiji.

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *