Msuya taja mbinu mpya kupaisha uchumi

Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa Msuya (aliyeketi) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

“SASA kitu ambacho watu hawaelewi, ningetaka hili mlielewe, ni watu wengi kufikiri matatizo ya uchumi yaliyotukumba (Tanzania) katika kipindi kile cha mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa 1980 mpaka pale Mwalimu Julius Nyerere alipotoka mwaka 1985, kwamba ni kwa sababu ya Ujamaa; wanavyosema sera ya ujamaa na viwanda haya, haikuwa ile.”

Hii ni kauli ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa Msuya akiweka rekodi sawa baada ya kuulizwa ni namna gani serikali, hasa yeye alipokuwa waziri wa viwanda, walimudu kujenga viwanda licha ya hali ngumu ya uchumi iliyokuwapo bila nchi kuwa na fedha.

Haya aliyabainisha wakati alipokuwa kizungumza katika mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) waliofika nyumbani kwake katika Kijiji cha Chomvu, Kata ya Usangi wilayani Mwanga, Kilimanjaro.

Advertisement

Katika mahojiano hayo, Msuya aliweka bayana mambo matatu yaliyosababisha hali mbaya ya uchumi katika kipindi alichoongoza Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda kwa miaka tofauti kabla ya kuwa Waziri Mkuu.

Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, alimteua kwa mara ya kwanza kuwa mbunge na kumpa uwaziri wa fedha mwaka 1972. Mwaka 1975, Nyerere alimteua tena kuwa mbunge na kumpa uwaziri wa viwanda hadi mwaka 1980.

“Aliponiteua kuwa Waziri wa Viwanda, nika survey potential (nikaangalia fursa) iliyopo. Nilirudi serikalini, nikasema bwana there is much we can do (kuna kitu zaidi tunachoweza kufanya), nikitazama serikali hatuna pesa, kitu kinachowezekana ni kujikita katika dhamana ya mikopo ya uagizaji.”

“Haya mataifa makubwa yana mikopo, ambayo inatolewa kwa sababu wanataka ku-export products (kusafirisha bidhaa zao nje ya nchi) zao. Kwa maana Mjapani anataka mashine zake za kushona nguo, tukikopa kule kuna kitu kinaitwa export guarantee system.
“Wanatupa kwa bei nafuu kidogo lakini si tough (yenye masharti magumu) kama ile ya commercial (biashara).

“Basi tukakubaliana hivyo. Ndiyo njia tuliyotumia. Maana kusema we use one money no money (maana hatuwezi kusema tunaweza kutumia fedha na hakuna fedha) ya kutosheleza hapa ndani, lazima mpate ile ya marafiki.

“Kwa mfano, Wachina walitupa Urafiki Textile (Kiwanda cha Nguo cha Urafiki) na Ubungo Farm Implements (Kiwanda cha Zana za Kilimo cha Ubungo-UFI).”

“Lakini ukitaka viwanda, tulijenga mfano Musoma, tukapanua Mwatex tukajenga vingine pale Tabora, Tabotex na Sunguratex. Inabidi kupata rasilimali kutoka nje. Na kikubwa ni kwamba uweze ku-guarantee (kuhakikisha) kwamba nitalipa,” anasema na kufafanua ukweli kuhusu sababu za matatizo ya uchumi yaliyoikumba nchi miaka hiyo ya 1970 na 1980.

Ujamaa si sababu

Msuya anataja mambo matatu yaliyotikisa uchumi kipindi hicho kuwa ni kupanda kwa bei ya mafuta kwa takribani asilimia 200, Vita ya Kagera na kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mafuta kupaa

“Kama hatuna watu ambao wanaweza kutathmini kujua ni nini kinachotokea duniani, tutakuwa tunababaika bure. Wakati ule, kwa wale ambao mnataka kusoma, OPEC (Nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani) waliongeza bei ya mafuta karibu asilimia 200,” anasema.

Anasema ongezeko hilo lililofanyika mwaka 1973 na 1979, liliumiza si tu Tanzania pekee, bali pia nchi  nyingine duniani ambazo fedha zote walizozalisha, zilielekezwa kwenye ankara za mafuta.

Alitoa mfano kuwa katika kipindi hicho alikwenda Jamaica na Tunisia na kwamba zote zilipitia katika tatizo hilo.

Vita ya Kagera

Kuhusu vita ya Kagera, Msuya anasema: nchi ilibidi kuazima silaha kutoka nje ili kumzuia Idd Amin wa Uganda kuvuka kwenye mpaka baada ya kutangaza kuwa eneo la Kagera ni lake.

Jumuiya kuvunjika

Akizungumzia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Msuya anasema wakati huo walikuwa Arusha katika mchakato wa kuunganisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Afro Shiraz Party (ASP), ikatangazwa kuhusu uamuzi wa Kenya ambayo ilizuia pia ndege.

“Sasa tunafanyaje? Tulibaki na ndege sijui mbili, tatu zilizokuwa nyumbani kwetu (Tanzania), tukazuia hizo.

Lakini impact(matokeo) kubwa ni kwamba, zile huduma zilikuwa zinaendeshwa na jumuiya.”

Ililazimu nchi kuanzisha vyombo vya kitaifa vya Kitanzania vinavyojitegemea kuendesha huduma hizo. Mfano, kwa upande wa reli, badala ya kutegemea East African Railway and Harbours (shirika la reli na Bandari la Afrika Mashariki), ilianzishwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendesha huduma za reli nchini.

Vivyo hivyo kwa Posta na pia utafiti ikizingatiwa kwamba kulikuwa na uliokuwa ukifanywa na jumuiya. Pia ilibidi nchi ianzishe mfumo wa kutoa mafunzo kwa wazawa ikiwamo mafunzo kwa marubani.

“Kwa hiyo, kitu ambacho mlikuwa mkishirikiana na wenzenu, kikivunjika, unarudi, inabidi muanzishe vya kwenu ili system (mfumo) iendelee,” anasema na kusisitiza kuwa, bei ya mafuta kupaa, gharama za vita na gharama za kuvunjia jumuiya ndiyo vitu vilivyodhoofisha uchumi.

“Kwa hiyo wale wanaosingizia ooh ni Ujamaa na nini na nini, ni ubabaishaji tu. Ukweli ni kwamba, ni tukio juu ya uwezo wa serikali yoyote ile.

“Na haya ninayotaja yote, ukiacha hasa hilo la vita na Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi zote zinazoendelea, zilikumbwa na matatizo hayo,” anasema na kutoa mfano wa Jamaica kwamba yalitokea maandamano.

Tofauti uchumi

wa sasa na zamani

Wakati huohuo; Msuya ameainisha mambo matatu yanayopaisha uchumi sasa kiasi cha kuwezesha nchi kuzalisha fedha za kigeni zaidi ikilinganishwa na kipindi chao cha uongozi.

Akilinganisha Tanzania ya zamani na sasa kiuchumi, Msuya anasema mapato ya nje kwa upande wa mazao ya kilimo, hayajabadilika. Hata hivyo, anasema ikiachwa mazao ya nafaka, anasema mazao ya biashara kama vile pamba na kahawa hayajazalishwa kwa wingi.

Kuhusu madini, anasema yamechangia mapato mengi na hivyo kufanya uchumi wa sasa wa Tanzania kuwa na ziada kubwa tofauti na zamani.

“Ndiyo sababu, Rais John Magufuli na Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) walikwenda kutia saini yale machimbo ya Nicol kule mpakani mwa Ngara na Rwanda na Burundi,” anasema.

Anauelezea uwapo wa madini adimu kuwa ni bahati nyingine ambayo Tanzania imejaaliwa sasa.

“Mungu ametujalia, hizi wanaita rarely metals (madini adimu)…ndizo bahati tunazo hizo. Hayako kila mahali… Tuna vitu ambavyo vimetuongezea kitu ambacho hatukutazamia.”

Jambo lingine linalotofautisha uchumi wa sasa na zamani kwa mujibu wa Msuya, ni uwapo wa gesi asilia mkoani Mtwara. Anasema ni faida kubwa kwani imeepusha uagizaji nje tofauti na kipindi chao.

Kingine alichotaja kuwa muhimu katika uchumi wa sasa ni makaa ya mawe, akihimiza nchi iyachangamkie sambamba na kuboresha miundombinu ya usafirishaji hususani kujenga reli.

“Lakini cha mwisho ambacho kimemea juzi juzi, na sijui kama watu wanakichangamkia, ni makaa. Kwa sababu, hivi vita vya huko Ulaya akina Ukraine na Urusi, mataifa yale makubwa yanataka kujihami na kukusanya makaa… ndiyo sababu pale Mtwara sasa hivi kuna meli zinakuja, zinataka kununua makaa.

“Wanaweza kuwa Wajerumani, Wahindi, Wachina. Nafikiri Waamerika watafufua makaa yao. Sasa shida yetu, haya makaa yako hapo Songea, huko Ludewa. Wanapeleka kwa maloria kutoka pale kwenda Mtwara, hiyo barabara itachakaa haraka sana,” anasema.

Anaongeza: “Kitu ambacho kingefanyika ni kupata reli, ijengwe haraka sana ili tuweze kusafirisha nje makaa zaidi kwenye miundombinu isiyoharibika. Sasa hii ni nyongeza, kitu ambacho hatukutarajia.”

Amesisitiza kuwa sambamba na juhudi za uzalishaji katika kilimo na viwanda, nchi ikielekeza nguvu zake kwenye mambo hayo matatu, itajenga uwezo kwenye fedha za kigeni.

 Katika hatua nyingine, Msuya amehimiza viongozi wa sasa na wataalamu kufanya utafiti juu ya namna ya kuendesha uchumi.

“Maana katika uchumi kuna yale mnayoyaweza ninyi ambayo yanawapeni nguvu. Lakini pia kuna yale yanayotokea nje ya uwezo wenu ambayo hamuyawezi mpaka mtafute njia za ku-survive (kuhimili).”