Mtanda ataka migogoro ya ardhi imalizike

MWANZA: MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wakazi wa kata ya Luchelele pamoja na viongozi wa Halmashauri wa Jiji la Mwanza kumaliza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiathiri maendeleo ya wananchi katika kata hiyo.

Mtanda amesema hayo leo Mei 19 wakati wa kusikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Nganza.

Mtanda amesisitiza kuwa migogoro hiyo imekuwa chanzo cha ucheleweshaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku baadhi ya wananchi wakishindwa kutumia ardhi yao ipasavyo kutokana na migogoro ya muda mrefu.

“Ni muhimu kwa wananchi kuwa na moyo wa maridhiano na kutafuta njia za kumaliza migogoro yao kwa mazungumzo badala ya kusubiri Serikali iingilie kati kila mara.” alisema.

Amewataka viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha hawawezi kuwa sehemu ya migogoro hiyo.

Akizungumzia hali ya migogoro katika eneo la Luchelele, alisema eneo hilo limekuwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi kutokana na kukosekana kwa mipango mizuri ya matumizi ya ardhi.

Alibainisha kuwa ni muhimu eneo hilo kupimwa na kupangwa vizuri ili wananchi waweze kumiliki maeneo yao kihalali na kuondoa migongano inayojitokeza mara kwa mara.

Mtanda alieleza kuwa upangaji bora wa maeneo pamoja na utoaji wa hati za umiliki utasaidia kuongeza thamani ya ardhi na kuwapa wananchi fursa ya kuwekeza na kupata maendeleo ya uhakika.

Pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wataalamu wa ardhi kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Igumilo kata ya Luchelele, John Josephat amesema kuwa migogoro mingi imekuwa ikisababisha hasara kubwa kwa familia pamoja na kuzorotesha shughuli za maendeleo katika jamii.

Ameiomba Serikali kusaidia kuwalipa fidia wakazi 150 wa mtaa wake kuweza kulipwa fidia kwakuwa eneo lao lilichukulia na Halmashauri ya Jiji ya Mwanza kwajili ya ujenzi wa eneo la kuchezea mchezo wa Golf.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Zena Kapama amekiri kumekuwa na mgogoro wa ardhi kwakuwa baadhi ya wananchi hawakujitokeza wakati wa ukaguzi hivyo hawakufanyiwa uthamini wa maeneo mbalimbali ya kata ya Luchelele.

Amesema baadhi ya wananchi waliofanyiwa uthamini kabla hawajalipwa fidia waliuza maeneo hayo kwa watu wengine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button