MWAKA 1991, Wakuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) wakati huo, walianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi uliotokea Juni 16, 1976 katika kitongoji cha Soweto, Afrika Kusini.
Wakati huo, wanafunzi watoto wadogo waliandamana kupinga mfumo na elimu duni waliyokuwa wanapatiwa, wakiitaka serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini kuboresha mfumo wa lugha ya kufundishia.
Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao wa Afrika Kusini katika kulinda utu, heshima na haki zao za msingi.
Watoto wanakumbushwa wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo kwa kuboreshewa hali na mazingira ya elimu kwao katika Afrika.
Siku hii inaadhimishwa kwa kuangalia maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inawapasa watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zao kushughulikia changamoto zinazokabili watoto katika Afrika nzima.
Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili na unyama wanaoweza kutendewa ndani na nje ya familia zao, wanapaswa kuepushwa na ndoa na mimba za utotoni kwa kupewa na kurithishwa maadili mema.
Wazazi wanapaswa kuwajibika kikamilifu kwa ulinzi na kuwatunza watoto wao na kuhakikisha wanapata mahitaji yao ya msingi na kwa wakati.
Watoto wafundishwe umuhimu wa kuwa na nidhamu katika maisha na walindwe vyema.
Hatua hizo zinapochukuliwa zitalenga jitihada za kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.
Kwa msingi huo, ipo haja ya kuhakikisha kwamba ‘hakuna mtoto anayeachwa nyuma’ kwa kuongeza nguvu kuwafikia watoto hasa wale wasiofaidika na kukua kwa maendeleo ya Tanzania.
Hivyo, wakati wowote wa kuandaa mipango na sera za kutekeleza Agenda 2030, watoto wanapaswa kuwa ndani ya mipango ili kuhakikisha hakuna mtoto anaachwa nyuma katika kuendesha maendeleo ya uchumi fungamani.
Wazazi wanawajibu wa kutambua kuwa familia ndio taasisi ya kwanza kuweka msingi wa maendeleo ya watoto kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa na mataifa yaliyo mengi.
Licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa kitaifa na kimataifa kuwalinda watoto, bado watoto wengi wamekuwa wakipitia magumu ikiwemo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Vitendo hivyo ni pamoja na utelekezwaji, vipigo, utumikishwaji wa kazi ngumu, mimba na ndoa za utotoni ambapo yote haya yanakatiza ndoto zao za kimakuzi na maendeleo.
Kwa kiwango kikubwa vitendo hivi hufanywa na ndugu, jamaa na wazazi na zinaweza kubadilishwa na walezi na wazazi hao.
Hivyo Siku ya Mtoto wa Afrika inawakumbusha viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa lolote hayawezi kupiga hatua bila kutilia maanani mahitaji ya watoto wakiwemo wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.
Mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hapa nchini yalibeba kaulimbiu isemayo: “Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu: Tumtunze, Tumlinde na Kumuendeleza”.
Takwimu zilizotolewa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro wakati wa Siku ya Familia Duniani, Mei 15, mwaka huu zilibainisha kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2023, vitendo vya ukatili vilivyoripotiwa viliongezeka kwa asilimia kubwa mkoani humo.
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoripotiwa katika madawati ya jinsia na watoto ya Polisi hufanywa zaidi kwa kundi la watoto na vijana wenye umri wa miaka 1-18 ambapo Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 100 yalikuwa ni ya mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Matukio 26 yalikuwa ni ya kutelekeza familia, 13 kutorosha wanafunzi, manane ya kujaribu kubaka na saba ni ya ukatili dhidi ya watoto.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Jesca Kagunila anaizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu kuwa inalenga kutoa elimu kwa wazazi, walezi na jamii kuhusu namna ya kuchukua hatua ya kuwalinda watoto na ukatili wa watoto mitandaoni.
Kagunila anasema taarifa ya utafiti wa hali ya ukatili mtandaoni ya mwaka 2021 katika nchi mbalimbali duniani inaonesha asilimia 67 ya watoto wenye umri kuanzia miaka 12- 17 ndio wanaopenda kutumia simu janja na mitandao ya intaneti.
Anasema kundi hilo linatumia simu za ndugu zao wa karibu wakiwemo wazazi, walezi, marafiki na ndugu wengine wa karibu wanaowazunguka.
Kagunila anasema, taarifa hiyo imeonesha asilimia nne ya watoto ni waathirika wakubwa wa kufanyiwa ukatili mitandaoni kulazimishwa kujihusisha na ngono, kusambazwa picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao.
“Ndiyo maana tunahimiza simu janja wasipewe watoto lakini kama ni mzazi lazima waangalie watoto wanavyotumia na wadadisi kwa mtoto kile anachokiangalia,” anasema Kagunila.
Kagunila anasema baadhi ya wazazi nchini wamekuwa wanawapa watoto simu na hawajishughulishi kujua wanaangalia mambo gani kwenye simu hizo.
Naye Ofisa Mipango wa Shirika lisilo la Kiserikali la Childhood Development Organisation (CDO), Innocent Rusomyo anasema ni wajibu wa wazazi na walezi kuwapa upendo, ulinzi na usalama watoto kwani wanapaswa kujisikia salama katika mazingira yao.
“Wazazi na walezi wanapaswa kumpa mtoto upendo, uangalizi na kuhakikisha ya kwamba wanajenga mazingira salama na yenye utulivu kwa ajili ya mtoto kujifunza na kukua,” anasema Rusomyo.
Askofu wa Kanisa la Pentekoste (EAGT) mkoani Morogoro, Dk Peter Dennis anaishauri jamii kuendelea kuimarisha maadili na upendo kwa familia ili kujenga malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Askofu Dk Peter anawaomba wazazi na walezi wawe wakali na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wanaowafanyia matendo maovu watoto wao hata kama wana mahusiano ya kindugu.