MSHITAKIWA, Khamisi Luwongo anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe, Naomi Marijani kisha kuuteketeza mwili wake kwa magunia ya mkaa na kuyafukia majivu, ameiomba Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu kumpatia nafasi ya kuonana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo.
Luwongo amewasilisha ombi hilo leo kwa Hakimu mkazi mkuu, Rhoda Ngimilanga baada ya kunyoosha mkono na kupewa nafasi ya kuzungumza, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendeshwa kwa njia ya mtandao (Video conference).
Akijibu ombi hilo, Ngimilanga amesema kuwa utaratibu uko wazi, hivyo anatakiwa kuandika barua kwenda kwa Hakimu mfawidhi kuomba miadi ya kuonana naye, yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo.
“Utaratibu uko wazi unatakiwa kuandika barua kwenda kwa Hakimu mfawidhi akiipata utajibiwa lini ana nafasi, ili ukaonane naye mimi sina mamlaka hiyo,” alisema.
Awali Wakili wa serikali, Faraja Nguka aliieleza Mahakama kuwa kesi hiyo iilikuwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 13, 2023 kwa ajili ya kutajwa.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Mei 15 mwaka 2019, eneo la Kigamboni Gezaulole, Khamisi alimuua mkewe, Naomi Marijani kisha kuuteketeze mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na kwenda kuyafukia majivu katika shamba lake, huku mgogoro katika ndoa yao ikidaiwa kuwa chanzo.