Mtwara mambo safi vitambulisho vya Taifa
MTWARA; UZINDUZI wa ugawaji wa vitambulisho zaidi ya 300,000 vya Taifa, umefanyika leo katika Kata ya Ufukoni Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amesema ugawaji huo ni kufuatia agizo la Rais Dk Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati alipofanya ziara hivi karibuni mkoani humo.
“Niwapongeze kwa dhati kabisa Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) na mkoa kwa ujumla kwa utekelezaji wa haraka agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa kwenu, juu ya upatikanaji wa vitambulisho kwa mikoa yote ya Tanzania iliyopo pembezoni na sisi Mtwara tukiwa wanufaika,”amesema Abbas.
Amewapongeza wananchi mkoani Mtwara kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo muhimu na la kihistoria ndani ya mkoa huo la ugawaji wa vitambulisho kwa idadi kubwa.
Ofisa Usajili wa Nida Mkoa wa Mtwara, Gide Magila amesema suala hilo ni endelevu, hivyo amewahamasisha wananchi wote waliokuwa bado kujisajili wafike kwenye ofisi za mitaa, vijiji kwa ajili ya kupata utaratibu wa awali wa kusajiliwa, ili na wao waweze kupata vitambulisho.