HALMASHAURI ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara imepanga kuandaa mikutano katika vijiji vyake vyote kuzungumza na wazazi kwa lengo la kuhakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza anaripoti na kuanza shuleni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella amesema mpango huo utaenda sambasamba na viongozi wa serikali ya halmashauri hiyo kwenda nyumba kwa nyumba, ili kubaini wanafunzi ambao bado hawajaripoti shulen.
“Sisi kama halmashauri tumejipanga viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji, wenyeviti wa vijiji, wetendaji wa vijiji na kata pamoja na maafisa elimu kata tunafanya mkutano na wazazi, lakini pia kwenda nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kuingia kidato cha kwanza anaenda shule,” amesema.
Yegella amesema mpaka kufika Januari 18, asilimia 60 ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza katika halmashauri hiyo wameshaanza shule.
Amesema katika mikutano hiyo , maafisa elimu kata watawaeleza wazazi umuhimu wa kupeleka watoto wao shule na mikakati ambayo serikali imefanya kuhakikisha kila mwanafunzi ambaye anajiunga na kidato cha kwanza anaenda shule na kupata elimu bila usumbufu.
Yegella amesema serikali imejenga madarasa 26 mapya kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari katika halmashauri hiyo.