Muheza waomba soko la matunda, viungo

TANGA, Muheza: MBUNGE wa Muheza, Hamis Mwinjuma amemuomba, Rais Samia Suluhu Hassan awasaidie kupata soko la kimataifa la machungwa na viungo.

Mwinjuma alisema wilaya hiyo ndiyo inayoongoza kwa kilimo cha mazao hayo kwa wingi lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa soko, hali inayosababisha wakulima kutonufaika na bei zisizo rasmi za uuzwaji wa mazao hayo.

“Machungwa na viungo changamoto kubwa ni soko lisilofahamika, hivyo tunaomba utusaidie soko la kimataifa la mazao hayo ili kuepuka madalali ambao wanawanyonya wakulima,” alisema Mwinjuma maarufu kama ‘Mwana FA’ ambaye pia, ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Alisema madalali wananunua machungwa mashambani kwa soko ambalo sio rasmi, hivyo uwepo wa soko la kimataifa utasaidia kudhibiti bei holela.

Aidha, alipongeza serikali kwa kuyarudisha kwa wananchi mashamba ya mkonge huku akiiomba serikali korona iliyopo kwenye Shamba la Kibaranga ikarabatiwe na kupewa halmashauri kusaidia ukusanyaji wa mapato.

Vilevile, alimshukuru Rais Samia kwa namna alivyoinua sekta ya elimu Muheza, akitolea mfano mwaka 2015 wilaya ilijenga madarasa 20 pekee wakati ndani ya miaka minne madarasa 219 ya shule za msingi yamejengwa na 109 katika ngazi ya sekondari.

Kwa upande wa maji, alisema katika miaka minne takwimu za upatikanaji wa huduma ya maji katika kipindi cha mwaka 2020 ilikuwa asilimia 41 na sasa imefikia 71%.

“Kwa vijiji wakati nakuwa mbunge wa jimbo hili mwaka 2020 asilimia ya maji ilikuwa 43 pekee na sasa imeweza kufikia asilimia 73 na mpaka Mradi wa Miji 28 utakapokamilika, haki ya upatikanaji maji itaweza kufikia asilimia 100,” alieleza mbunge huyo ambaye pia, amewahi kuwa msanii maarufu nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button