Muhimbili imekidhi vigezo AFCON 2027

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imefuzu kuwa na uwezo wa kushughulikia dharura za kiafya zinazoweza kujitokeza katika michuano ya  Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ikiwa Afrika Mashariki itapewa ridhaa ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Haya yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakub ambaye aliambatana na jopo la wakaguzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ambao wapo nchini kukagua miundombinu muhimu ikiwemo viwanja vya michezo, hoteli, uwanja wa ndege na hospitali.

Advertisement

“Katika ukaguzi huo leo wamefika Hospitali ya Taifa Muhimbili,  ambapo wamekagua idara ya magonjwa ya dharura na ajali, mashine za kisasa za uchunguzi lakini pia wamepata maelezo mazuri kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi, ambaye ameeleza uwezo na utayari wa MNH katika kutatua dharura zozote zinazoweza kujitokeza,” amesema Yakub.

Amesema ukaguzi unakwenda vizuri na kwamba Muhimbili imekidhi vigezo vilivyotakiwa na zinasubiriwa tu baadhi ya nyaraka ambazo wakaguzi hao wameziomba.

Awali akiwasilisha mada kwa wakaguzi hao, Prof.  Janabi alisema kuwa Muhimbili ndio hospitali kubwa nchini, ikiwa na vitanda 2,150 katika kampasi zake za Upanga na Mloganzila,  huku ikiwa na wataalamu bingwa wa kada zote, ina mashine za vipimo vya uchunguzi ikiwemo MRI 3, CT Scan 3, Angio Suit 1 pamoja na idara ya magonjwa ya dharura yenye uwezo wa kuhudumia watu wapatao 250 kwa siku.

“Kijiografia katika eneo iliyopo Hospitali yetu kuna Hospitali mbili za ubingwa wa juu ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), ambazo kwa pamoja zina uwezo wa kutatua changamoto yoyote inayoweza kujitokeza,” ameeleza Prof. Janabi.

Kwa upande wa jopo la wakaguzi wa CAF wakiongozwa na Lakshmikanthi Karunanithi kwa kiasi kikubwa wameoneshwa kuridhika na ubora wa huduma na miundombinu iliyopo MNH.

Tanzania imeomba kuwa mwenyeji wa  mashindano ya AFCON 2027  kwa kushirikiana na nchi jirani ambazo ni Kenya na Uganda.

 

6 comments

Comments are closed.

/* */