Mulokozi kuzindua mradi mpya wa elimu

DAR ES SALAAM; MKURUGENZI wa Kampuni ya Mati Super Brand Limited, David Mulokozi amesema yupo katika mpango wa kuzindua mradi mpya wa elimu kwa vijana, ambao ni sehemu ya jitihada za kurudisha kwa jamii.

Imekuwa ni utamaduni wa kiongozi huyo kurudisha kwa jamii, ambapo mara kadhaa amekuwa akifanya hivyo akiamini jamii inahitaji watu wenye uhitaji inapaswa kuangaliwa kwa ukaribu.

Akizungumza na HabariLEO, Mulokozi amesema mradi huo utajikita katika kuwapa vijana mafunzo ya kiufundi na ujasiriamali, ili kuwawezesha kujiajiri na kuanzisha biashara zao wenyewe.

“Tutatoa mikopo midogo kwa watakaoonesha ubunifu na mipango mizuri ya biashara. Lengo kuu ni kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujifunza na kujipatia kipato kupitia kazi zao wenyewe,” amesema..

Amesema amekuwa akitoa ushauri kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kurudisha kwa jamii na kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za kijamii, ili kufikia walengwa kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.

“Nawaeleza kuwa biashara zao zitakua na kudumu zaidi ikiwa jamii inayowazunguka itanufaika na uwepo wao. Nasisitiza kuwa kurudisha kwa jamii sio tu suala la kijamii, bali ni mkakati mzuri wa kibiashara unaojenga uhusiano mzuri na wateja na kuongeza uaminifu kwa bidhaa au huduma zao,” amesema.

Oktoba 21, 2023 alitoa fimbo nyeupe 500 kwa watu wasioona ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali, lakini pia Juni 20, 2022 alikabidhi vitakasa mikono kwa taasisi za serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button