MAHAKAMA ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu imemkuta na kesi ya kujibu mwalimu Subiri Edson,37, wa shule ya Sekondari Nguno iliyopo katika wilaya hiyo anayetuhumiwa kwa kosa la kumbaka mwanafunzi, 17, nyumbani kwake.
Uhamuzu huo mdogo umetolewa leo na hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Hakimu Mfawidhi Mkazi wa Mahakama hiyo, Robert Kaanwa mara baada ya kusikiliza mashahidi sita na kielelezo kimoja kutoka upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo namba 28803/2024, mshtakiwa atatakiwa kuanza kujitetea kwa kuwasilisha mashahidi wake au kutoa ushahidi wake wa kiapo kwa mujibu wa kifungu cha 231 cha makosa ya jinai.
Hakimu Kaanwa ametoa uhamuzi huo mdogo, kwa mujibu wa kifungu cha 231 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
SOMA: Jela miaka 30 kwa kumbaka ajuza
Awali akitoa maelezo ya kosa la mshtakiwa, mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Jaston Mhule amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 07/2024.
Amesema alilitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 (1)(2) e na 131(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Amesema katika kijiji hicho cha Nguno wilayani humo maeneo ya sekondari anakofundisha, mshitakiwa alimbaka mwanafunzi wa sekondari chumbani kwake.
SOMA: Baba mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mwanaye Geita
Aliendelea kueleza kuwa tarehe hiyo mshtakiwa aliwekwa chini ya ulinzi wa wananchi baada ya kumkamatwa akiwa na mhanga chumbani kwake majira ya saa moja usiku na baada ya kumkamata walimfikisha kituo cha polisi Itilima.
Hakimu Robert Kaanmwa amehairisha kesi hiyo hadi Oktoba 21, 2024 ambapo kesi hiyo itatajwa tena kwa ajili ya kuanza kusikiliza utetezi kutoka upande wa mshatakiwa.