Mwalimu aliyemuua mwenzake ajinyonga

MWALIMU wa Shule ya Msingi Igaka Kata ya Isulabutundwe, Tarafa ya Kasamwa wilayani Geita, Samwel Abel anayetuhumiwa kumuua mwalimu mwenzake, Emmanuel Chacha (35) amekufa kwa kujinyonga akiwa mahabusu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo alisema kabla ya kujiua mtuhumiwa alihojiwa na alikiri kufanya tukio hilo na alieleza sababu ni ugomvi wa kugombania nafasi na baada ya mahojiano mtuhumiwa alirejeshwa mahabusu.

“Siku ya Machi 17, 2023 majira ya saa 10 alfajiri mmoja wa mahabusu alienda chooni na kumkuta Samwel Abel ambaye ni mtuhumiwa wa tukio hilo akiwa ananing’inia chooni,” alisema Kamanda Jongo alipozungumza na waandishi wa habari.

Advertisement

Alisema mtuhumiwa alijinyonga kwa kutumia shati alilokuwa amelivaa kwa kujitundika kwenye nondo za dirisha la choo cha mahabusu.

“Juhudi zilifanyika za kumchukua na kumpeleka hospitali kwa sababu alikuwa hajafa bado lakini hatima yake alipoteza maisha akiwa hospitali,” alisema Kamanda Jongo.

Wakati huo huo Kamanda Jongo alisema uchunguzi wa tukio la kufukuliwa kaburi umefanyika na kubaini mbali na kaburi hilo kukutwa limefukuliwa kwa kiwango fulani jeneza na mwili havikuibwa.

“Siku ya Machi 17, 2023 nilipata taarifa kutoka kwa waandishi wa habari kwamba mtoto wa miaka miwili amefukuliwa huko Lwamugasa lakini sisi kama Jeshi la Polisi hatukuwa na taarifa hiyo,” alisema na kuongeza:

“Mhusika alikiri kutueleza tukio hilo la kaburi na mtoto wake kufukuliwa, aliyekuwa amezikwa Februari 15, 2023. Lakini Februari 16, 2023 watu walioenda malaloni wakakuta kaburi la mtoto wake limefukuliwa, lakini baada ya mahojiano yake ya kina alikiri kuwa hajawahi kutoa taarifa kituo cha polisi.”

Alisema Machi 17, 2023 Jeshi la Polisi liliomba kibali cha mahakama ili kuthibitisha madai ya baba wa mtoto kuwa kaburi la mwanawe limefukuliwa na mtoto kuibwa ambapo hatua za uchunguzi zilifanyika.

“Tulifukua kaburi ambapo tulikuta jeneza la mwili huo likiwa halijawahi kufunguliwa, na tulifungua hilo jeneza na tulikuta mwili wa huyo mtoto umelala vizuri na haujakatwa kiungo chochote,” alisema Kamanda Jongo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *