Mwanaharakati anayetamani kila mwenye haki apate haki

“NAKUMBUKA nilikuwa nalia kabisa ninapoona mtu ananyanyaswa, nilikuwa napata uchungu ninaposikiliza kesi ya mtu aliyedhulumiwa na anapeleka kesi mpaka mahakama kuu na wengine hukata rufaa Mahakama ya Rufani lakini anashindwa kesi, kwa sababu nilikuwa mwanasheria mchanga niliivaa ile kesi basi nilikuwa naumia,” anasema Anna Henga.

Anna ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), nafasi anayoiongoza tangu mwaka 2019, ni Wakili wa Tanzania na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mwanaharakati huyu ni mtoto wa pili kati ya sita wa familia ya marehemu Aloys Henga na mama Sophia ambao kwa pamoja walikuwa watumishi wa umma, baba akiwa mchumi na mama akiwa katibu muhtasi katika uwanja wa ndege.

Mbali na kuwa mke na mama wa mtoto mmoja wa kike, pia ni mchungaji msaidizi anayesaidiana na mchungaji mkuu kuongoza waumini wao katika kanisa.

Anna ambaye anajinasibu kuwa mwanakwaya mzuri, pia ni Mwenyekiti wa Kwaya ya Glorius Cathedral na anatumia muda wake mwingi kanisani kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali baada ya kazi zake, ni sehemu ya kutulia na kufurahia na watu wengine.

Anasema amekuwa akishiriki kuimba wakati wa jioni na kuhudhuria kwenye mikesha kanisani kitu ambacho anaeleza kukipenda zaidi kwa kuwa kinamsaidia kutokana na kazi anayofanya na kujiweka sawa kisaikolojia.

Anna anasema wakati anasoma alipenda kuwa mtangazaji kwenye redio kabla ya kuanza kwa luninga na kwamba alikuwa mpenzi wa kusikiliza Redio Tanzania wakati huo, sasa ikiitwa TBC FM na kwamba alipomaliza kidato cha sita, alikuwa na machaguo matatu ikiwemo kuwa mwanasheria, mwandishi wa habari na mtaalamu wa sosholojia.

Anasema kuwa marehemu baba yake alimshauri kusomea sheria lakini wakati huo alikuwa hafahamu masuala yoyote kuhusu sheria na kwamba kutokana na ufaulu mzuri alipokuwa sekondari aliomba kusomea sheria.

“Nakumbuka wakati ule kujiunga na sheria ilikuwa lazima ufaulu vizuri kwa maana ya kuwa na daraja la kwanza unapomaliza kidato cha sita na kwa sababu nilikuwa na vigezo vyote, nilisoma na kuanza kuipenda fani hii nikaona ni kitu kizuri,” anasema.

Safari yake ya utetezi wa haki za binadamu Anaeleza kuwa wakati yuko chuoni alijiunga na klabu ya haki za binadamu ya chuo hicho, hivyo alikuwa akivutiwa zaidi na vitu walivyokuwa wanafanya katika kutetea haki za wanafunzi na kujiapiza kwamba anatamani kufanya kazi kwenye mashirika ya haki za binadamu.

Anasema kuwa zamani ilikuwa lazima kwa wanafunzi wa sheria kwenda kufanya kazi kwenye mashirika au kampuni za uwakili baada ya kumaliza mwaka wa nne ili kupata mafunzo kwa vitendo ndipo wafanyiwe sherehe za kuhitimu.

“Mimi niliomba nifanye mafunzo yangu katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Ofisi ya Arusha kwa sababu nilikuwa nakaa huko, niliomba kujitolea na nilipomaliza nilirudi shuleni na nikarudi tena kituoni hapo kujitolea bure kabisa kwa sababu nilipenda kutetea watu,” anasema. Anna anaongeza kuwa baada ya kufanya vizuri aliajiriwa na kuanza kazi ya kutoa msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ikiwemo waliodhulumiwa haki zao kwa kuwaandikia nyaraka za kwenda mahakamani. Anasema kuwa wakati anaanza kufanya kazi hizo alikuwa akijiingiza kwenye kesi kama mlalamikaji hivyo kuchangia kupatwa na uchungu mwingi pale anapoona watu walionyanyaswa wanashindwa kesi.

Kwa mujibu wa Anna, baada ya kuwa mtaalamu katika fani hiyo, alianza kufanya kazi zake bila kujiingiza kwenye kesi anazopokea na baadaye alihamishwa kitengo cha jinsia cha LHRC na kuanza kushughulikia masuala ya wanawake ambao wakati huo walikuwa duni na wenye hali ya chini. Anasema wanawake wamekuwa wakidhalilishwa kiasi kwamba hata matusi yanayotamkwa na watu mbalimbali hususani kwenye usafiri wa umma yanahusisha viungo vya mwanamke jambo ambalo lilikuwa linamkera.

“Niliwahi kufanya kipindi kimoja cha haki za wanawake, nilizungumza sana kuhusu matusi yanayomdhalilisha mwanamke na wengi waliniunga mkono, kwa tafiti zetu za sasa angalau kuna unafuu kwani mwanamke ameanza kuheshimiwa na zaidi imechangiwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” anafafanua na anaongeza kuwa uwakili na uanaharakati ni vitu viwili tofauti kwa sababu mawakili hufanya biashara kwani baada ya kuhudumia wateja wao hulipwa.

Anna anasema wanaharaka- ti hawalipwi na wateja bali kuna wafadhili ambao huwachangia gharama za uendeshaji ili kuwasaidia wananchi na kwamba hutetea haki za binadamu mahali popote na bila kuagizwa. Anasema licha ya kwamba wanaharakati wengi ni mawakili lakini sio kila wakili ni mwanaharakati.

Kitu asichoweza kusahau Anna anasema kuwa hatasahau siku moja akiwa na polisi walipokwenda kumkamata mwanamume mmoja wa kabila la Kikurya aliyekuwa analazimisha kumkeketa mke wake. “Nilienda kijijini kabisa huko ndani ndani tukamkamata huyo baba na kumpeleka polisi, na alifunguliwa mashitaka,” anasema na anaongeza kuwa tukio hilo liliwezesha kupata tuzo iliyotolewa na mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Melania Trump na Katibu wa Ikulu, Mike Pompeo.

Tuzo hiyo ya Kimataifa ya Wanawake Jasiri aliipata mwaka 2019 kwa kutambua juhudi zake kati- ka kutetea haki za wanawake na watoto nchini Tanzania. Wanawake wengine waliopata tuzo hiyo ni kutoka nchi za Bangladesh, Djibouti, Misri, Ireland, Jordan, Montenegro, Myanmar, Peru na Sri Lanka. Katika hafla hiyo, serikali ilitambua kazi na ujasiri uliooneshwa na wanawake hao katika kushawishi, kuongoza na kuleta matokeo chanya yaliyobadilisha jamii licha ya kuhatarisha maisha yao na kujitoa muhanga.

Anaeleza kuwa yapo mambo mengi yanayoendelea nchini ambayo hawezi kuyasahau. Nafasi yake LHRC Wakili huyo anasema nafasi ya ANNA HENGA Mwanaharakati anayetamani kila mwenye haki apate haki Ukurugenzi wa LHRC hakuchaguliwa badala yake aliomba nafasi hiyo. Anasema kuwa wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa kituo hicho, Hellen Kijo Bisimba alipokuwa anakaribia kustaafu, kituo kilitangaza nafasi hiyo naye alituma maombi ya ajira.

Anna anasema alikuwa na wenzake wengine ambao waliomba kwenye nafasi hiyo na kwamba walifanyiwa usaili na kushinda. “Baada ya kupata ajira hii nilikuwa na furaha iliyochanganyika na wasiwasi namna nitakavyofanya kazi zangu. Nilijiona nina mzigo mkubwa kwa sababu nafasi hii ni kubwa na inaangaliwa na watu wa makundi mbalimbali ikiwemo watumishi wa umma, wanawake, wanasiasa, wakulima, wafugaji na watoto wakitegemea kuwa utawatetea,” anasema.

Pia anaeleza kuwa alikuwa akifanya kazi hiyo kwa saa 80 kwa wiki badala ya 40 na kwamba alishauriwa kupunguza muda wa kazi ili kutodhuru afya yake. Anasema alikuwa anafanya kazi nyingi akilenga kutaka kumsaidia kila mtu anayehitaji msaada wake na kila anapopata taarifa kwenye vyombo vya habari anapenda kuvifanyia kazi.

Anna anasema kazi hiyo sio nyepesi lakini ni nzuri pale wanapoona watu wanapata haki zao kwa sababu wamewasaidia. Anasema baadhi ya changamoto anazopitia ni kutoeleweka katika jamii hususani wanawake wanaotetea haki za binadamu na kupimwa kama wanafamilia au la kueleza kuwa wanafahamu wanachokifanya.

Anna anasema changamoto nyingine ni kituo hicho kuonekana kinapinga serikali na kuna wakati wananyimwa vibali vya kufanya kazi kwa sababu wanahisiwa kuwa na mrengo fulani wakati sio kweli. Anasema, “ukweli ni kwamba sisi tupo katikati tunatetea mtu yeyote anayeonewa.” Anasisitiza kuwa changamoto ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ukatili wa jinsia na malezi ni makubwa na ripoti za haki za binadamu kwa miaka minne mfululizo inaonesha kuwa ukatili kwa watoto unaongoza kutokana na wazazi na walezi kusahau jukumu lao la malezi na kuwaacha watoto wakijilea wenyewe.

Anna anaeleza kuwa wazazi wamekuwa na shughuli nyingi za kutafuta fedha na kuwasahau watoto wao na wanapogundua tatizo tayari wanakuta mtoto ameshaharibika na anaongeza kuwa wana jukumu la kuhakikisha kwamba wanawalea watoto kwa kufuata sheria na sera zilizopo.

“Sera ya mtoto na sheria zimekaa vizuri kwa asilimia 80, hivyo zikitekelezwa ipasavyo watoto watapona kutoka katika ukatili,” anasisitiza Anna. Kuelekea siku ya wanawake Anna anatoa wito kwa wanawake mwezi huu wa Machi wahakikishe wanatetea haki za watoto wa kike, wanawake na wanaume ili waweze kulinda haki hizo.

Anasema wasikubali kuonewa na kunyamaza bila kuzungumza na kusisitiza kuwa taasisi za umma na binafsi zihakikishe zinafanya ujumuishaji wa jinsia,” anasema na anaongeza kuwa kituo hicho kimefanikiwa kupata tuzo ya ujumuishaji jinsia kwa kuwa taarifa zao na miundombinu iko vizuri kwenye masuala ya jinsia na kwamba wanafundisha kuhusu bajeti za jinsia hivyo aliwakaribisha watu kujifunza suala hilo.

Anna ameidhinishwa kuwa Mjumbe wa bodi mbalimbali za ndani ya nchi na Kimataifa ikiwemo kuwa Mdhamini wa Baraza la Kikristo Tanzania, amekuwa mjumbe wa mashirika ya kimataifa ya Mpango wa Washirika wa Kitaalamu juu ya Ushirikiano wa Kiraia Jumuishi na Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Afrika.

Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti mwenza wa Kikundi cha Ushauri cha Mashirika ya Kiraia Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDPTanzania), Makamu Mwenyekiti wa UN Global Compact Tanzania, Mjumbe wa Bodi Shule ya Sekondari Urafiki na Mjumbe wa bodi na Mjumbe wa Kamati Ndogo za Maadili na Ukaguzi Baraza la Habari Tanzania (MCT). Wakili huyo amekuwa akibuni na kusimamia programu mbalimbali za kuimarisha ulinzi na kukuza haki za wanawake nchini Tanzania. Vilevile shirika analoliongoza limepokea tuzo mbalimbali za programu za kujumuisha jinsia ndani na nje (2021 na 2022) wakati Juni 2019, alianzisha mpango unaoendelea wa ‘Programu ya Ushauri kwa Wanafunzi wa Kike’ ili kuwawezesha wasichana wachanga shuleni na vyuo vikuu juu ya haki zao. Mwaka 2011, alifanya kazi kuweka muktadha wa Itifaki ya Maputo, 2003 ili maudhui ya itifaki hiyo yapatikane kwa Watanzania wengi.

Pia amefanya kazi kama mratibu wa Muungano wa Kupambana na Ukeketaji Tanzania na kufanikiwa kuishirikisha jumuiya ya Waislamu chini ya Baraza la Waislamu Tanzania kukanusha dhana iliyokuwepo kwamba wanaunga mkono ukeketaji.

Anna pia amefanya kazi ya kuwawezesha wanawake kutambua haki za ardhi hasa katika kushawishi muundo wa wanawake katika mabaraza ya ardhi na pia amechangia kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika uchaguzi kupitia uwezeshaji wa haki za kisiasa. Mwaka 2010, alifundisha wanawake wanaotaka siasa nchini Tanzania chini ya UNIFEM (sasa UN Women).

Anna ana shahada ya uzamili ya Sera ya Maendeleo na Utendaji kwa Asasi za Kiraia ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tanzania, Stashahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara iliyotolewa na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Stashahada ya Jinsia- kutoka Taasisi ya Utawala wa Umma na Stashahada ya Theolojia kutoka Shule ya Theolojia ya Sweden na Wizara ya Mahanaim na Cheti cha Utawala Bora

Habari Zifananazo

Back to top button