Mwandishi HabariLeo ang’ara Tuzo za Sayansi
DAR ES SALAAM: MWANDISHI wa gazeti la HabariLeo, Lucy Ngowi ameibuka kidedea na kuwa mshindi wa jumla katika tuzo ya mashindano ya umahiri na uandishi wa habari za sayansi iliyotolewa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Tuzo hiyo imetolewa usiku wa kuamkia Jumamosi katika ukumbi wa Costech mkoani Dar es Salaam, ambapo Lucy amekuwa mshindi wa jumla akifuatiwa na Elias Msuya wa Gazeti la Mwananchi ambaye alipata ushindi wa kuandika habari za sayansi wakati wote.
Akizunguza kabla ya kukabidhi tuzo katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu amesema tume inajivunia waandishi wa habari wanaohabarisha masuala ya sayansi na teknolojia jambo ambalo ni muhimu.
“Tunapokuwa na waandishi wanaoweza kuandika kwa ufasaha ni jambo jema. Sayansi na Teknolojia zinaongeza tija kwenye kilimo. Ni lazima sayansi na teknolojia itumike katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi ambayo yanachochea ukame na visumbufu mbalimbali katika mazao,” amesema Nungu.
Amesema wanasayansi wanapofanya utafiti wao vizuri na taarifa zikafika kwa wakulima, watalima kwa tija kwa kutumia sayansi na teknolojia.
“Kufanya kazi Costech na waandishi ni jambo ambalo halikwepeki.
Tunaendelea kuwaenzi,” amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (Ofab), Dk Philbert Ninyondi amesema miaka saba iliyopita wamekuwa wakifanya mashindano ya umahiri na waandishi wa habari za sayansi kwa tume hiyo kutoa tangazo ambalo liliwataka waandishi kuwasilisha kazi zao.
Amesema mwaka huu utaratibu huo umebadilika na kuangalia taarifa za sayansi zinachapishwa na waandishi kila wiki ama kila mwezi nak ujua mwandishi huyo ameandika nini ama chombo cha habari kimechapisha ama kutangaza taarifa zipi.
“Baada ya kufuatilia kwa utaratibu huo kazi hiyo walipewa majaji, tume ikaona ni nani amefanya nini na majaji kuangalia yule anayestahili kupata tuzo hiyo,” amesema.
Kwa upande wake Lucy amemshukuru Mungu kwa tuzo hiyo na kuishukuru kampuni anayoifanyia kazi ya Magazeti ya Serikali inayochapisha Dailynews na HabariLeo, costech kwa kuratibu mafunzo mbalimbali kwa waandishi pamoja na watafiti mbalimbali kutoka vyuo vikuu vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) cha Morogoro.
“Ushindi huu sio wangu peke yangu bali ni ushindi wa TSN, Costech na watafiti mbalimbali,” amesema na kushauri waandishi kutokata tamaa kuandika habari za sayansi katika kilimo hususan za bioteknolojia katika ulimwengu wa sasa wenye changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.