‘Mwanzo wa kifo cha ukanjanja umetimia’

DAR ES SALAAM; BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imezinduliwa rasmi leo, huku Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando, akisema huo ni mwanzo wa kifo cha ukanjanja kwenye uandishi wa habari.
Akizungumza Dar es Salaam leo baada ya uzinduzi huo, Mhando amesema kwa kushirikiana na wenzake kwenye bodi hiyo watafanya kila njia kuhakikisha wanasimamia weledi na masuala yote yalipo kwenye sharia iliyoanzisha bodi hiyo.
Uzinduzi wa bodi hiyo umefanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa pamoja na wadau mbalimbali wa habari.
Bodi hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229, ikiwa na jukumu kuu la kutoa ithibati kwa waandishi wa habari hapa nchini.
Waziri Kabudi katika maelezo yake alisema bodi hiyo ni chombo muhimu katika kusimamia viwango vya taaluma ya uandishi wa habari, kuhakikisha uzingatiaji wa maadili ya kitaaluma, pamoja na kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuboresha weledi wao.



