Mwekezaji Anne Marie Academy amwagiwa sifa

MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Dk Jasson Rweikiza (CCM),  amepongezwa kwa kuwekeza kwenye elimu na kusaidia jitihada za serikali kuboresha sekta hiyo nchini.

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid, wakati wa mahafali ya darasa la saba ya Shule ya St Anne Marie Academy ambapo jumla ya wahitimu 230 walitunukiwa vyeti.

Maulid alisema amefurahishwa na ubora wa elimu unaotolewa na shule hiyo ambayo imekuwa ikiongoza Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ubungo na kuingia kwenye kumi bora kitaifa mara kwa mara.

“Kuna usemi kwamba usione vyaelea vimeundwa, maana umahiri wa wanafunzi niliouona hapa ni jitihada za walimu na menejimenti ya shule nawapongeza sana, shule ziko nyingi sana ila nimeamua kuja hapa St Anne Marie kwa sababu hakuna longolongo hapa,” alisema na kuongeza:

“Mimi ni Ofisa Elimu wa Mkoa, mkuu wangu wa mkoa anajua leo St Anne Marie kuna nini, ameniambia nije hapa na pia kuna Mkurugenzi wa Halmashauri, kuna Ofisa Elimu wa Wilaya hapa, mheshimiwa diwani naye yupo hapa, kwanini, kwa sababu wazazi mmechagua shule bora na hamjakosea kuwaleta watoto wenu hapa.”

Aliwataka wazazi kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na wasimwamini mtu kuhusu ulinzi wa watoto wao kwani vitendo vya ukatili dhidi yao vimekuwa vingi.

Pia aliwataka wamiliki wa shule wahakikishe mabasi yanayobeba wanafunzi yanakuwa salama na aliwataka wapeleke mabasi hayo yakakaguliwe.

Aliwataka wamiliki wa shule kuacha kuwarundika wanafunzi kwenye basi moja, badala yake wanunue mabasi mengi ili wanafunzi wasibanane kupita kiasi.

“Hata wadhibiti ubora uliowaajiri ndio wamesababisha matokeo mazuri hapa shuleni kwenu ndiyo maana nawataka wengine waje wajifunze St Anne Marie maana haya matokeo hayajaja kutoka hewani tu,” alisema.

Alitoa wito kwa shule kuacha kuwachuja wanafunzi kwa kisingizio kwamba wamefanya vibaya kwenye masomo hali ambayo inawapa msongo wa mawazo wazazi.

Aliwataka wamiliki wa shule zote kuhakikisha hawawazuii kufanya mitihani ya mwisho kwa kisingizio hawajalipa ada kwani sheria na sera ya elimu hairuhusu.

Aliwapongeza wazazi kwa kuendelea kuwasomesha watoto wao akisema kuwa hakuna urithi mzuri kama elimu kwani ni hazina anayoishi nayo miaka yote.

Mkuu wa shule hiyo, Gladius Ndyetabura alisema matarajio yao ni kuendelea kuwa kwenye 10 bora kitaifa na kuendelea kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ubungo katika matokeo ya kitaifa.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button