Mwendokasi ya gesi Dar kuanza Aprili

KAMPUNI ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) imesema inatarajia kupokea mabasi 100 kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Mkurugenzi Mkuu wa Udart, Waziri Kindamba kupitia ujumbe uliowekwa kwenye ukurasa wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), amesema mabasi hayo yanatumia gesi.

“Kwa hiyo Aprili 2025, tutapokea gari la kwanza la majaribio lakini ni matumaini yetu pia kwamba yale mengine 99 sasa yatafika kabla ya mwaka wa serikali 2024/2025 kupinduka,” alisema Kindamba.

Advertisement

Alisema mabasi hayo yanatengenezwa China na akasema mengi yanayotumika sasa yamechoka hivyo yanahitaji kubadilishwa.

“Swali linaweza kuja kutoka kwa Mtanzania kwa nini yamechoka katika miaka tisa hadi kumi, ukweli ni kwamba magari haya yanafanya kazi siku saba za wiki, masaa takribani 24 kwa sababu yanaanza saa 10 alfajiri mpaka saa sita za usiku,” alifafanua Kindamba.

Aliongeza: “Kwa hiyo ni magari ambayo yapo kwenye kazi wakati wote ‘day in day out’, kwa hiyo inawezekana kabisa yapo baadhi ya magari machache yakawa na mapungufu ya hapa na pale ndio maana kama menejimenti mpya tumeamua kufanya maamuzi ya kuleta magari mapya yanayotumia teknolojia ya gesi iliyosindikwa”.

Desemba mwaka jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema serikali ilikuwa kwenye mchakato wa kununua mabasi 100.

Chalamila alisema ni muhimu kuongeza mabasi ya mwendokasi kulingana na mahitaji, na alitoa mfano kuwa miradi ya Kimara na Mbagala inahitaji zaidi ya mabasi 770 ili kutosheleza mahitaji ya usafiri kwenye maeneo hayo.

Aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 300 kwa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo kwa haraka katika mkoa huo.

Chalamila alisema barabara hizo zinazojengwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama za serikali na wafadhili zinapokamilika hukabidhiwa kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambaye naye huingia makubaliano na mtoa huduma ambaye ni Kampuni ya UDA Rapid Transit Public Limited Company (UDART) ili kuendesha miradi hiyo na kutoa huduma za usafiri kwa wananchi.

Alisema kuna maoni kuhusu umuhimu wa kuongeza watoa huduma watakaoweza kuongeza mabasi kwa ubia na serikali kwenye baadhi ya barabara zinazojengwa sasa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *