MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salam, Khadija Ally, amesema hataki watu ambao kazi yao ni kujipendekeza ‘chawa’, badala yake anataka viongozi na wanachama wa jumuiya hiyo kuchapa kazi.
Akizungumza leo Desemba 14, 2022, ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, Khadija amesema yeye sio Mwenyekiti wa chawa na kutaka viongozi na wanachama wa jumuiya hiyo kufanya kazi kuanzia ngazi ya Kata, kuangalia malezi ya watoto, maadili na elimu katika shule zinazomilikiwa na jumuiya hiyo.
“Tufanye kazi zionekane, jamii ifaidike, tuwe viongozi wenye maadili, viongozi tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa, hatuwezi kuwa viongozi ambao hatuna maadili,” amesema.
Kufuatia hali hiyo, Khadija amesema anaandaa mafunzo maalum ya uongozi na kukumbushana misingi ya jumuiya, maadili ya uongozi na malezi.
“Sisi hatuwezi kuwa na kiongozi asiye na maadili, tuwe na uongozi shirikishi sio uongozi wa kimungu, utakachosema ndio hicho hicho hutaki ushauri, hutaki kusikia lolote kwa mtu yoyote, hapana! Uongozi lazima uwe shirikisho,” amesema.
Chawa ni msemo ulijichukulia jina katika jamii siku za karibuni, ukimaanisha watu wenye tabia za kumganda mtu mwingine, kujipendekeza na kumsifia kwa nia ya kufaidika naye.
Pia katika kikao hicho ulifanyika uchaguzi mdogo wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya jumuiya hiyo, ambapo walioshinda nafasi ya Baraza la Mkoa na Kamati ya Utekelezaji Wazazi Mkoa ni Omar Ngurangwa, Muhammad Abdulghafur na Busoro Pazi.