Mwigulu ‘atikisa’ matumizi serikalini

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameielekeza Wizara ya Fedha kuyapitia mafungu ya fedha yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali na kwamba ambayo matumizi yake hayaathiri shughuli za msingi yakatwe, yapelekwe kwenye miradi.

Dk Mwigulu alisema hayo mkoani Mwanza wakati akizindua meli ya MV New Mwanza. Aliongeza kuwa, mafungu pekee ambayo hayataguswa ni yale yanayohusu vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na afya.

Alieleza kuwa yapo mafungu katika wizara ambayo matumizi yake hayaathiri shughuli za msingi kama ununuzi wa magari, sherehe, kadi, kalenda, maua na vinywaji.

“Yeyote mwenye hamu ya kunywa soda akanunue anywe kwake suala la tarehe na kalenda mnaweza kutumia kalenda za simu,” alisema.

Alisisitiza, “tunataka fedha hizo tuzipeleke kwenye miradi iliyosimama kutokana na mkandarasi kukosa fedha za awali. Kateni! Zipo fedha ambazo mkiziondoa huko hatuathiriki.”

Tanzania haiendeshwi kwa rimoti

Sambamba na hayo, Dk Mwigulu aliwashangaa wanaharakati wanaokataa suala la maridhiano na kubainisha kwamba Tanzania haiendeshwi kwa rimoti.

SOMA: Mambo safi MV Mwanza

Akiweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa vituo vya maji katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Dk Mwigulu alisema wanaharakati hao wamekosa mwelekeo.

Alisema wanaharakati hao hawastahili heshima kwa sababu wamedhamiria kuliangamiza taifa na kwamba kwa sasa wanatapatapa kwa sababu mirija yao iliyokuwa ikiwapa kiburi imekatwa.

Alibainisha kuwa ni jambo la ajabu kwa wanaharakati ambao hawaishi Tanzania wala hawanufaiki na amani ya nchini, kukataa azma ya serikali ya kuwa na maridhiano miongoni mwa Watanzania.

“Nilimsikiliza mwanaharakati mmoja anasema hatutaki maridhiano, wewe mwanaharakati hata Tanzania haupo hata hapa hauishi wala ndugu zako hawaishi hapa unasema hutaki maridhiano kwani tunaridhiana na wewe kuhusu nini,” alihoji Dk Mwigulu.

Aliongeza kuwa wanaharakati hao mirija yao ilikatwa na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli na baadaye
wakaanzisha mtandao wa kumtukana na kufikia hatua ya kufanya sherehe alipofariki.

Alisema tabia yao inakiuka misingi ya Kitanzania, hivyo kutostahili heshima. Kuhusu utekelezaji wa miradi nchini, Dk Mwigulu alisema kuwa Tanzania ni Tajiri kwani inao uwezo wa kutumia rasilimali zake na fedha za ndani kukamilisha miradi yake.

“Miradi hii ni kwa ajili ya maendeleo yenu. Tunahitaji uwajibikaji na mshikamano. Watendaji wote wanapaswa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” alisema.

Mradi huo umegharimu Sh bilioni 46.2 ukiwa umekusudiwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi 450,000 wa Jiji la Mwanza na wilaya za Magu na Misungwi.

Maeneo yatakayonufaika kwa kuhakikisha huduma ya maji safi, salama na ya uhakika yanapatikana kwa kila mwananchi ni Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyahingi, Luchelele, Sahwa, Kishiri, Igoma, Kisesa, Bujora, Kanyama, Fela na Usagara.

Kadhalika, Dk Mwigulu alitolea mfano wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwamba fedha za kuikamilisha mpaka Mwanza zipo tayari kinachosubiriwa ni mkandarasi kukamilisha ili apewe fedha zake.

“Siku si nyingi zijazo tutakunywa chai Mwanza, chakula cha mchana tutakula Dodoma na chakula cha jioni tutakula mkoani Dar es Salaam,” aliongeza Dk Mwigulu.

Wakati huohuo, aliwataka wananchi wa Kanda ya Ziwa kuwapeleka watoto wote walioandikishwa shule ili kuwajenga viongozi wazuri.

Ampa ‘rungu’ Mbarawa
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwelekeza Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuwafukuza kazi watumishi wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji (MRCC) watakaobainika kusababisha madhara kwa kusinzia au kuchati na simu zao.

Aliongeza kuwa litakuwa ni jambo la aibu na laana maafa yakitokea wakati nchi ikiwa na vifaa vya kisasa vya uokozi. Alisema serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza katika eneo la kuokoa maisha ya Watanzania.

“Rai yangu kwenu, kwa wale watendaji watakaosimamia jambo hili, linahusisha masuala ya kidharuradharura wasisinzie wala wasifanye mzaha kwa sababu wakisinzia kidogo tu inaathiri maisha ya watu wanaokwenda majini,” alisema Dk Mwigulu.

Aidha, Dk Mwigulu alisema kwa kawaida mtendaji akizembea kuwaambia watu wanaoingia ziwani kuwa ziwa limechafuka atakuwa amesababisha matatizo kwa uzembe wakati taifa lina vifaa vya kisasa vya kuweza kuona yote yajayo katika siku inayofuata.

“Hao watakaokaa hapo, wajue wapo katika kazi inayozingatia uhai wa Watanzania; masaa ya kazi unatakiwa kuzingatia kazi, muda wa kupumzika na muda ambao upo nje ya kazi ndiyo unatakiwa kufanya mambo mengine,” alisisitiza Dk Mwigulu.

Aliongeza, “na hii ni kazi inayowataka muwe macho muda wote, ikitokea mtu akapigiwa simu ya dharura halafu akashindwa kuipokea kwa sababu amesinzia, mtu wa namna hiyo mheshimiwa waziri fukuza aondoke kabisa kwa sababu hii ni kazi inayomtaka mtu azingatie na atoe msaada kwa wakati,”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button