Mwigulu: Watendaji msizoee shida za wananchi

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza watendaji waache kuzoea matatizo ya wananchi na kuyaona ni salamu za kawaida.
Dk Mwigulu ameyasema hayo Lushoto mkoani Tanga akiendelea na ziara kutembelea miradi ya maendeleo, kukwamua iliyokwama na kusikiliza wananchi.
“Haya hayakubaliki, pale Korogwe mkandarasi amechukua zaidi ya bilioni moja, anadunda mtaani na hajatekeleza mradi. Katika kumfuata wanasema inabidi kumchunguza, nimeagiza akamatwe asiwe huru hadi zipatikane hizo hela,” alisema Dk Mwigulu ambaye amekuwa Tanga kwa ziara ya siku tano.
Alisema viongozi wa mkoa na wilaya wapo na hata mamlaka nyingine zinafahamu ila hakuna hatua iliyochukuliwa, hivyo kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Mkuu wa Usalama Mkoa kumsaka mtuhumiwa huyo na kumkamata.
SOMA: Waziri Mkuu anusa wizi mwingine Muheza
“Kuna mambo yanasababisha lawama kwa viongozi wakuu kumbe wao walishatimiza wajibu wao, serikali imeshapeleka fedha kutekeleza mradi ila wahusika wameipiga hiyo hela na hatua hazichukuliwi. Kazi yao ni viingereza vingi, hatuwezi kutoa haki kwa wenye fedha na wanyonge wasipate haki, hapana! Halikubaliki,” alisisitiza Dk Mwigulu.
Hivyo, aliwataka viongozi kutafuta suluhu ya matatizo ya wananchi badala ya kuyazoea na matokeo yake yamekuwa mengi na makubwa bila sababu za msingi.
Aidha, alitoa pia maelekezo ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa ubakaji aliyembaka mwanafunzi mwenye umri wa chini ya miaka 18 na kusababisha akatize masomo kulea mtoto aliyetokana na ubakaji.
“Jana (juzi) nilikuwa pale Tanga, kuna kesi ya mtoto alilalamika kubakwa na mzee mwenye miaka 53 na akampa mimba na ameshajifungua, mtuhumiwa yuko huru anadunda,” alisema Dk Mwigulu.
Hivyo, aliagiza mtuhumiwa asakwe, akamatwe na sheria ifuate mkondo wake kama inavyoeleza adhabu ya mbakaji, kwani hata vipimo vya vinasaba (DNA) vilibaini vinasaba vya mtoto vinalandana na vya mtuhumiwa
lakini cha kushangaza hadi leo mtuhumiwa anadunda.
“Kesi ya mbakaji lazima irudiwe upya mahakamani. Mbakaji ana miaka 53 na huyo mtoto ana chini ya miaka 18, na ameshajifungua. Kamanda wa Takukuru na RSO (Ofisa Usalama wa Mkoa) wafuatilieni wale wote walioshika hilo jalada tujue, haiwezekani wananchi wa kawaida wateseke kwa kuwa hawana fedha, hiyo haiwezekani. Huyo asakwe na ripoti yake niipate,” aliagiza Waziri Mkuu.
Aidha, aliagiza pia watumishi wote waliocheza na hilo jalada nao wachunguzwe na taarifa ya watumishi hao wa umma imfikie na waunganishwe kwenye kesi hiyo.
Akijibu kero ya ukosefu wa baadhi ya dawa muhimu katika hospitali za wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Japhet Simeo alisema katika sekta ya afya, huduma za tiba kwa watoto ambao mapafu yao hayakukua vizuri awali haikutolewa katika hospitali hizo, bali ilipatikana hospitali za rufaa na mkoa.
“Ni kweli tiba na dawa kwa watoto waliozaliwa ambao mapafu yao hayakukua vizuri ilikuwa haitolewi katika hospitali za ngazi hii ila tumeshaiingiza kwenye huduma za msingi za afya na tayari dawa zinapatikana kwa ngazi hiyo, kama hatua ya kuboresha huduma za tiba kwa jamii,” alisema Dk Simeo.
Baada ya kusikia hilo, Dk Mwigulu aliwaagiza waganga wakuu nchini kote kuhakikisha tiba kwa watoto hao inapatikana katika hospitali za wilaya kwenye majengo ya mama na mtoto ili kusaidia jamii kupata huduma maeneo ya karibu.
“Rais Samia ameshachukua hatua kwenye sekta ya afya, inawezekana lisitekelezwe kwa asilimia 100 kila eneo lakini limeanza na tutaendelea kuboresha, kama ilivyo suala la kipimo cha MRI ambacho sasa kinapatikana katika hospitali zote za mikoa, kanda na rufaa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amewaonya na kuzuia leseni za uchimbaji madini kwenye maeneo ya makazi Magamba wilayani Lushoto, na kusema haiwezekani zimetolewa leseni zaidi ya 43 za uchimbaji kwenye eneo la makazi.
“Haiwezekani leseni zaidi ya leseni 43 zimetolewa kwenye eneo la makazi, hilo nimesitisha na limeisha,” alieleza.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, amezitaka taasisi za serikali nchini kote kuwa na hatimiliki za ardhi za maeneo yao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Alisema hayo baada ya mwananchi kutoa kero yake akisema eneo la familia wanalolilima kwa tangu mwaka 1970 serikali ya Wilaya ya Lushoto inataka kulichukua na tayari ameshaamriwa kuondoka.
Akieleza mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye alisema ni kweli analijua na kuwa eneo la serikali wilayani hapo halijapimwa ila wako katika kupitia upya mipaka na kuwa eneo la mlalamikaji
limo ndani ya eneo hilo.
Hivyo, Dk Mwigulu alisema haiwezekani taasisi za serikali zina maeneo yasiyo na hatimiliki hadi leo na kuagiza taasisi hizo nchi mzima kuhakikisha maeneo yake yote yanapimwa na kuwa na hatimiliki ili kuepusha migogoro.



