MTANGAZAJI na mwigizaji maarufu nchini Mwemba Burton ‘Mwijaku’ ameandika barua kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumuomba afute tuzo zinazotolewa kiholela na baadhi ya taasisi nchini, nyingi zikikiuka katiba ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mwijaku ambaye pia, ni mtangazaji wa Crown Media amesema kuwa tuzo hizo zina ukiukwaji wa misingi na taratibu za utoaji wa tuzo kama inavyobainisha katiba ya nchi.
Amesema akiwa kama mshindwanishaji wa baadhi ya vipengele na Watanzania wenzake ameona kuna baadhi ya taasisi zinazohusika katika utoaji wa tuzo hizo zikiwa na nia ovu za kuharibu majina au biashara za watu katika utoaji wa tuzo hizi hapa.
“Mfano kuna taasisi hushirikiana kutoa tuzo huku wakijua kuna baadhi ya vipengele husika vinawahusu wamiliki au wafanyakazi husika katika tuzo hizo na kusababisha maslahi binafsi katika utoaji tuzo hizo,”amesema.
Amesema kitendo hicho ni kinyume na taratibu za utoaji tuzo kwani kuna nia ovu ya watoa tuzo kudidimiza baadhi ya taasisi na ‘brand’ ya taasisi za watu ili kujinufaisha wao binafsi bila kujali gharama za washindanishwa husika namna walivyopambana kuzijenga kampuni au biashara husika.
Hata hivyo, kauli ya Mwijaku inakuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya kukosa tuzo alizokuwa anawania za Consumer Choice Awards ambapo alikuwa anagombea kipengele cha mhamasishaji bora sambamba na mpinzani wake Revocatus Chipando ‘Babalevo’ ambaye alishinda.
Mwigizahi huyo amesema atapita kwa wafanyabiashara Kariakoo Jumatatu kupeleka dodoso ili wasaini wakifika 100 atapeleka Bungeni ipigiwe kura na serikali ichukue.