Mwili wa Mkono kuletwa kesho, kuzikwa Jumatatu

MWILI wa wakili maarufu nchini, Nimrod Mkono (80) unatarajiwa kufikishwa Dar es Salaam kesho.

Taarifa zimeeleza kuwa mwili unatarajiwa kupokewa saa 10 alfajiri kutoka Marekani, utapelekwa nyumbani kwake Masaki na kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 8 mchana kutakuwa na ibada katika Kanisa la Waadventisti Wasabato.

Ratiba inaonesha kuwa keshokutwa waombolezaji wakiwamo viongozi wa kitaifa wanatarajiwa kuuaga mwili wa Mkono katika Viwanja vya Karimjee wilayani Ilala.

Aidha, siku hiyo jioni mwili utasafirishwa kwa ndege kupelekwa Mwanza na usiku utasafirishwa kupelekwa Busegwe.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kamati ya Mazishi, mwili wa Mkono utazikwa Mei 29, mwaka huu nyumbani kwake Kigori- Busegwe wilayani Butiama katika Mkoa wa Mara.

Mkono aliaga dunia Aprili 18, mwaka huu nchini Marekani wakati akiendelea na matibabu.

Mkono mbali na shughuli zake za uwakili, alikuwa Mbunge wa Musoma Vijijini tangu mwaka 2000 hadi mwaka 2015 na pia Mbunge wa Butiama kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020.

 

Habari Zifananazo

Back to top button