Mzize aandaliwa kuvaa viatu vya Samatta

Taifa Stars

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco amesema anamtengeneza mshambuliaji Clement Mzize, kurithi nafasi ya nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta.

Kauli hiyo ni baada ya Mzize kuonekana atika mchezo na Zambia wa kufuzu kombe la Dunia 2026, amevaa jezi namba 10 anayoivaa Samatta anayedaiwa anahitaji kupumzika kuichezea Stars na kupisha vijana kupambania taifa katika mashindano yaliyopo mbele yao.

Kwa mujibu wa Morocco,  Mzize ameonesha kiwango kizuri kwenye mechi na Zambia na ana uwezo mkubwa licha ya kutopata nafasi, anaamini mshambuliaji huyo akitengenezwa vizuri atakuja kuwa mrithi wa Samatta ndani ya kikosi cha Stars.

Advertisement

“Mchezaji mzuri ana uwezo wa kupanda na kusumbua wapinzani, changamoto ilikuwa kupata namba, matumaini yangu ni kuendelea kumjenga uwanjani kuja kuvaa viatu vya Samatta hapo baadae,” amesema kocha huyo.

Ameongeza kuwa mchezo dhidi ya Zambia ulikuwa mgumu na kulazimika kuwatumia wachezaji wengi wanaocheza soka la ndani kulingana na aina ya mchezo huo na kufanikiwa kupata ushindi.

“Niwaponge wachezaji wote wamepambana na kufanya yale niliyowapa uwanja wa mazoezi, walipambana na kujitoa na kutumia nafasi dakika za mwanzo na kufanikiwa kupata bao, walichokionesha tunaweza kukutana na yoyote na kufanya vizuri,” amesema Morocco.

Tanzania ipo kundi E,  ambapo vinara ni Morocco wenye pointi 6 baada ya kucheza mechi mbili huku Tanzania ikiwa nafasi ya pili na pointi 6 baada ya kucheza mechi tatu, Niger nafasi ya tatu, Zambia nafasi ya nne zina pointi tatu huku Congo ikiwa haina pointi..