NACTVET wasisitiza kozi zenye tija kwa jamii

KATIBU Mtendaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dk Adolf Rutayuga amevitaka vyuo mbalimbali hapa nchini kuacha kutoa kozi za mazoea ambazo zinajirudia katika vyuo vingi na badala yake watoe kozi zinazoweza kuleta manufaa ya haraka kwa jamiii ili kujenga uchumi endelevu.

Dk Rutayuga ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya awamu ya tatu kwa wamiliki na wakuu wa vyuo binafsi vya Mafunzo ya Ufundi Stadi toka Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa mkoani Morogoro.

“Tanzania tumekua tukitoa kozi zilezile za zamani kama vile mpiga chapa (Typist), ushonaji, umeme wa majumbani na nyinginezo,lakini naomba sasa tuziangalie jamii zinazotunguzuka na kuona ni jinsi gani tunaweza kutoa kozi ambazo zinaweza kuzisaidia jamii zetu kuboresha kile wanachokifanya kuwa na tija na kuongeza kipato.” amesema Rutayaga.

Amesisitiza ni lazima wajiulize kwa pamoja je kuna chuo chochote kinachofundisha wafugaji jinsi ya kuweza kuhifadhi majani kipindi cha masika ambayo yangeweza kuwasaidia wakati wa ukame au mafunzo ya kuwawezesha wakulima kupunguza matumizi ya madawa kwenye bidhaa za mbogamboga na matunda ili kulinda afya za walaji.

Pia amewataka wadau wote wa elimu ya ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi kushirikiana ili kujenga nguvukazi yenye ujuzi na umahiri na kuwaaasa wamiliki na wakuu wa vyuo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyowekwa na NACTVET ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi mapungufu mbalimbali yaliyoainishwa katika vyuo vyao kwa maendeleo ya ufundi stadi nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button