Nafasi ya kilimo cha chai katika uchumi Tanzania

TANZANIA ni nchi ya pili kwa uzalishaji zao la chai Afrika ikitanguliwa na Kenya. Sekta ya chai ina wakulima wadogo 32,000 na mashamba makubwa ya chai 12.

Takwimu zinaonesha Desemba hadi Machi mwaka huu, mauzo ya chai yameliingizia taifa Sh bilioni 50.25, kupitia vibali vilivyotolewa na Bodi ya Chai Tanzania (TTB) kusafirisha nje ya nchi.

Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji chai, mwaka 2022/2023 uzalishaji ulikuwa tani 26,754. Mwaka 2023/2024 uzalishaji ulikuwa tani 20,845 na mwaka 2024/2025 lengo ni kuzalisha tani 30,000 lakini uzalishaji ulikuwa tani 22,772.

Kwa mujibu wa TTB, wakulima wadogo huzalisha takribani asilimia 40 ya majani mabichi ya chai nchini. Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wilaya za Mufindi, Njombe na Rungwe ndiyo inayozalisha chai zaidi ikichukua zaidi ya asilimia 80 ya uzalishaji wote nchini.

Kanda ya Kaskazini Mashariki (wilaya za Lushoto, Korogwe na Muheza) inachangia karibu asilimia 20 huku Kanda  ya Kaskazini Magharibi (wilaya za Bukoba na Muleba) ikichangia kwa asilimia ndogo.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Zao la Chai hivi karibuni jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anasema serikali imeweka mikakati ikiwemo kuongeza thamani ya zao la chai nchini kwa kuhamasisha uuzaji wa chai iliyochakatwa badala ya chaighafi kuwezesha wakulima kunufaika kupitia vyama vya ushirika.

Anasisitiza umuhimu wa kuboresha mchakato wa uzalishaji wa chai kushindana kimataifa kutokana na soko la chai kukua kwa kasi na kuwa na fursa kubwa za kiuchumi. Anahimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa na mafunzo kwa wakulima kuongeza uzalishaji na viwango vya ubora.

“Tukifanya kazi pamoja, tunaweza kufikia malengo yetu na kuleta maendeleo katika sekta hii ya zao la chai,” anasema. Anasema kufanikisha hilo, TTB imenunua mashine tatu kati ya saba zilizopangwa kununuliwa katika mwaka huu wa fedha.

Hatua hii itasaidia kukabiliana na changamoto ya soko kutokana na kufungwa kwa viwanda vya Mohamed Enterprises Ltd (MeTL) na Marvella. “Kama hatua ya mwanzo, mashine mbili ya kuchakata na kuchanganya chai zitafungwa katika eneo la Dindira, Korogwe na kukabidhiwa kwa wakulima wadogo kupitia AMCOS kwa makubaliano maalumu na Bodi ya Chai,” anasema Bashe.

Aidha, bodi imenunua mashine ya kuchanganya chai na nyingine ya kufungasha zitakazofungwa katika ghala kuwezesha wanunuzi kuongeza thamani ya chai inayonunuliwa mnadani, hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.

Bashe anasema Bodi ya Chai imebuni chapa ya taifa ya chai ya Tanzania na kuwataka wadau wote wakiwemo wachakataji, wafungashaji na wachanganyaji kutumia chapa hiyo katika vifungashio vyao ili kutambulika kitaifa na kimataifa. “Chai yetu imekuwa ikiuzwa na mataifa mengine bila kufahamika kuwa ni ya Tanzania. Kupitia chapa yetu, sasa chai yetu itatambulika popote inapouzwa,” anasema.

Kwa mujibu wa Bashe, Serikali kupitia TTB imefungua masoko ya chai katika nchi za Oman, Qatar, Dubai, Japan na Saudi Arabia. Aidha, Kiwanda cha Mponde Holdings kimesaini mkataba na Kampuni ya Mumtaz ya Oman ambayo kuanzia sasa itanunua tani 100 kila mwezi.

Aidha, wanunuzi kutoka Urusi na Dubai wameomba kuunganishwa na kiwanda hicho kwa mkataba wa tani 260 kila mwezi, Kampuni ya Kazi Yetu nayo imesaini mkataba wa kuuza chai maalumu nchini Qatar. Anasema hadi  kufikia Machi 25, 2025, mauzo ya chai yameiingizia taifa Sh bilioni 50.25 kuanzia Desemba hadi Machi, mwaka huu kupitia vibali vilivyotolewa na TTB kusafirisha nje.

Kwa mujibu wa Bashe, serikali inatekeleza shughuli mbalimbali kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025 pamoja na
miradi ukiwamo Mradi wa Ustahimilivu wa Usalama wa Chakula uliowezesha kuwapo mazingira wezeshi ya uwekezaji wa sekta hiyo katika maeneo ya Kilolo, Njombe na Mbeya.

Miongoni mwa wawekezaji hao ni Kampuni ya ITO EN ya Japan inayonunua majani mabichi kutoka shamba la pamoja la NOSC na kampuni ya Hong Ding Xin Investment Limited iliyoanzisha kiwanda cha kuchakata chai maalumu Kilolo.

Hata hivyo, Waziri Bashe anabainisha changamoto zinazoikumba tasnia hiyo zikiwemo kushuka bei ya chai kimataifa kutokana na vita katika maeneo ya Ulaya Mashariki, Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini pamoja na uhaba wa Dola za Marekani katika baadhi ya masoko ya mbali kama Pakistan na India.

Kukabiliana na changamoto hizo, Bashe anasema serikali imeanza na wakulima wadogo wa Korogwe kwa kuwapa mashine za kuchakata na kuchanganya chai na kuendelea na jitihada za kupunguza tozo na kodi ikiwemo kuondoa kodi ya AMT kwa miaka mitatu hadi Juni 2027 na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa viwanda vya kuchanganya chai.

Anahimiza wachakataji kuwekeza katika teknolojia ya kisasa kupunguza gharama za uzalishaji, hasa matumizi
ya kuni, badala yake watumie nishati safi kama gesi na umeme wa jua. TTB inaendelea na uzalishaji wa miche bora ya chai kuziba mapengo shambani na kuondoa miche ya zamani isiyo na tija.

“Katika kuimarisha biashara ya chai, Bodi imeendelea kusimamia mnada wa chai wa Dar es Salaam ulioanzishwa Novemba 2023,  naofanyika kila Jumatatukwa kuongeza madalali na kuimarisha miundombinu ya Kipawa huku ikitafuta masoko mapya ya kimataifa,” anasema.

Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania (TTB), Beatrice Banzi anasema, “Kuna viwanda 22 vya kuchakata majani mabichi ya chai…. Kati ya hivyo 17, ndivyo vinafanya kazi.” Anasema biashara ya chai inafanyika kwa namna mbili, ikiwemo kuuza nje ya nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button